Misri yataka UN iingilie kati mzozo wa bwawa la al-Nahdha
(last modified Sat, 20 Jun 2020 06:47:06 GMT )
Jun 20, 2020 06:47 UTC
  • Misri yataka UN iingilie kati mzozo wa bwawa la al-Nahdha

Misri imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liingilie kati kwa ajili ya kutatua mgogoro wa bwawa la al-Nahdha la nchini Ethiopia.

Taarifa iliyotolewa jana Ijumaa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imesema, "Jamhuri ya Kiarabu ya Misri imeliomba Baraza la Usalama liingilie kati na kuanzisha mazungumzo mapya kuhusu mgogoro wa bwawa la al-Nahdha, baada ya kukwama mazungumzo hayo kutokana na mielekeo hasi ya Ethiopia."

Hii ni baada ya mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea huko Addis Ababa kati ya nchi hiyo, Ethiopia na Sudan kuhusiana na bwawa hilo kuvunjika tena hivi karibuni baada ya pande husika kushindwa kufikia makubaliano.

Haya yanajiri siku chache baada ya Naibu Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Ethiopia kutishia kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Misri akisisitiza kuwa, nchi hiyo ya Pembe ya Afrika itatetea kwa nguvu zake maslahi yake katika bwawa hilo.

Mradi wa bwala la al-Nahdha unahesabiwa kuwa mradi mkubwa zaidi wa umeme barani Afrika

Nchi mbili za Misri na Sudan zinapinga mradi wa ujenzi wa bwawa la al-Nahdha juu ya maji ya Mto Nile zikisema kuwa, ujenzi huo unapunguza mgao wa maji wa nchi hizo. 

Bwawa la al-Nahdha linajengwa katika Mto Nile nchini Ethiopia na katika umbali wa kilomita 40 kutoka mpaka wa Sudan. Ethiopia ilianza kujenga bwawa hilo mwezi Apili mwaka 2011, hata hivyo hitilafu kali kati yake na Misri na Sudan zimechelewesha ujenzi wake. 

Tags