Rais wa Misri aliamuru jeshi kuandaa oparesheni nje ya nchi
(last modified Sun, 21 Jun 2020 08:15:46 GMT )
Jun 21, 2020 08:15 UTC
  • Rais wa Misri aliamuru jeshi kuandaa oparesheni nje ya nchi

Rais Abdel Fattah el-Sisi ameliamuru jeshi la Misri kujitayarisha kutekeleza oparesheni ndani na nje ya nchi kwa lengo la kulinda usalama wa taifa huku hali ya taharuki ikiongezeka baina ya nchi hiyo na Uturuki kuhusu kadhia ya Libya.

El-Sisi amewaonya wanajeshi wa Serikali ya Muafaka wa Kitaifa ya Libya (GNA), ambayo inaungwa mkono kimataifa, wasivuke mstari wa sasa wa kivita baina yao na wapiganaji wa jenerali muasi Khalifa Haftar ambaye anaongoza kundi la wanamgambo wanaojiita Jeshi la Kitaifa la Libya (LNA).

Uturuki inaunga mkono Serikali ya Muafaka wa Kitaifa ya Libya na imeisaidia serikali hiyo kusambaratisha hujuma za wapiganaji wa Haftar ambao walikuwa wanakaribia kuuchukua mji mkuu, Tripoli. Wapiganaji wa Haftar wanapata uungaji mkono wa Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri, baadhi ya nchi za Magharibi na Russia.

Siku ya Jumamosi El-Sisi alitembelea uwanja wa ndege za kivita karibu na mpaka wa Misri na Libya ambapo alishuhudia mazoezi ya kijeshi.

 El-Sisi amedai kuwa Misri inaunga mkono suluhisho la kisiasa Libya na kuongeza kuwa hali sasa imebadilika huku akiashiria kuwa nchi yake iko tayari kutuma wanajeshi Libya. Wakati huo huo, Uturuki imesema wapiganaji wa Haftar mashariki mwa Libya wanapaswa kuondoka katika mji wa kistratijia wa Sirte ili kuweze kufikiwa makubaliano ya usitishaji vita. Rais wa Misri naye ameutaja mji huo kuwa mstari mwekundu ambao haupaswi kuvukwa na wanajeshi wa GNA.

Wakati huo huo, Uturuki inasema mpango wa Misri wa usitishwaji vita nchini Libya unalenga kumuokoa Haftar ambaye ameshindwa vibaya katika wiki za hivi karibuni.

Libya ilitumbukia katika machafuko na vita vya ndani baada ya wanajeshi wa Marekani wakishirikiana na wale wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kuishambulia nchi hiyo na kusaidia harakati za kumuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.

 

Tags