UN yataka Somalia isaidiwe kukabiliana na COVID-19
Mjumbe maalum wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia ametoa wito wa kutolewa misaada zaidi ya kimataifa kwa Somalia ili kuisaidia kukabiliana na janga la COVID-19 au corona.
James Swan amesema misaada iliyotolewa na washirika wa dunia yote imeiwezesha Somalia kutoa vifaa vya matibabu kwa wagonjwa wa COVID-19.
Bw. Swan ametoa taarifa baada ya kutembelea Hospitali ya De Martini huko Mogadishu, ambapo amepongeza juhudi za wafanyakazi wa afya na kusifu mwitikio wa haraka wa serikali ya Somalia kwa dharura ya afya ya umma ya COVID-19.
Hospitali ya De Martini imekuwa kituo kikuu cha kupima, kugundua maambukizi na kuwatibu wagonjwa mahututi wa COVID-19 nchini Somalia. Hospitali hiyo ina vitanda 71 vilivyotengwa kwa ajili ya wagonjwa wa COVID-19 na mashine 16 za kupumulia, pamoja na kituo cha karantini.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Somalia, jumla ya kesi 2,799 za COVID-19 zimeripotiwa nchini humo ambapo hadi sasa watu 90 wamefariki na wengine 782 wamepona baada ya kupata matibabu.