Raia 18 wa Misri watiwa mbaroni nchini Libya
(last modified Mon, 22 Jun 2020 07:42:14 GMT )
Jun 22, 2020 07:42 UTC
  • Raia 18 wa Misri watiwa mbaroni nchini Libya

Timu ya opereseheni za "Volkano ya Hasira" ya Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya imetangaza habari ya kutiwa mbaroni raia 18 wa Misri ambao ni wananchi wa kundi moja linaloendesha shughuli zake kinyume cha sheria nchini Libya.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, jana jioni timu hiyo ilitoa taarifa na kusema kuwa, raia hao wa Misri wametiwa mbaroni katika mji wa Sabratah wa magharibi mwa mji mkuu Tripoli. Taarifa ya timu hiyo ya operesheni za kijeshi ya Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya imeongeza kuwa, raia hao 18 wa Misri wamekabidhiwa kwa maafisa husika wa serikali kabla ya kufukuzwa nchini Libya. Hata hivyo duru za Misri zimekanusha habari hiyo na kudai ni ya uongo.

Kwa mujibu wa duru hizo za Misri, ukurasa wa mtandao ya kijamii wa Facebook wa al Wifaq  ambao ndio uliotangaza habari hiyo, umedukuliwa na kuchapishwa habari hiyo. Ikumbukwe kuwa Misri ni muungaji mkono wa jenerali muasi Khalifa Haftar, wanayeongoza kundi la wanamgambo wanaojiita "Jeshi la Taifa la Libya."

Mpaka wa Libya na Misri

 

Tangu mwaka 2015 mgogoro wa Libya umegeuka kuwa uwanja wa ushindani wa madola mbalimbali ajinabi. Baadhi ya madola hayo yanaiunga mkono Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa iliyoundwa kwa usimamiaji wa Umoja wa Mataifa na wengine wanamuunga mkono jenerali muasi Khalifa Haftar anayeongoza wanamgambo wanaojiita "Jeshi la Taifa la Libya."

Tangu mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka jana 2019, kundi la Khalifa Haftar lilianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya mji mkuu wa Libya, Tripoli kwa tamaa ya kuiangusha Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa.

Algeria nayo imetangaza kuwa, kwa vile ina mpaka mrefu na Libya unaokadiriwa kufikia kilomita elfu moja, ni jukumu lake kuzipatanisha pande hasimu za Libya na kupinga uingiliaji wowote wa madola ya kigeni, kwani matukio ya Libya yanaiathiri moja kwa moja Algeria.

Tags