Jeshi la Somalia laangamiza makumi ya wanamgambo wa al-Shabaab
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i61757-jeshi_la_somalia_laangamiza_makumi_ya_wanamgambo_wa_al_shabaab
Wanachama wasiopungua 27 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab wameuawa katika operesheni kadhaa zilizofanywa na jeshi la Somalia katika eneo la Shebelle Kusini mwa nchi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 22, 2020 07:48 UTC
  • Jeshi la Somalia laangamiza makumi ya wanamgambo wa al-Shabaab

Wanachama wasiopungua 27 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab wameuawa katika operesheni kadhaa zilizofanywa na jeshi la Somalia katika eneo la Shebelle Kusini mwa nchi.

Afisa wa jeshi la Somalia, Jenerali Abdihamid Muhammed Dirir amesema wanamgambo hao wameuawa katika operesheni tofauti zilizofanywa na jeshi hilo katika mji wa Dug Garir.

Amesema makamanda wawili wa ngazi za juu wa genge hilo ni miongoni mwa magaidi walioangamizwa katika operesheni hiyo na kusisitiza kuwa jeshi la Somalia limedhamiria kuendeleza operesheni zake dhidi ya wanamgambo hao.

Haya yanajiri baada ya watu saba wakiwemo wanajeshi wa serikali kuuawa katika mashambulizi mawili tofauti ya mabomu yanayoaminika kufanywa na kundi hilo la kigaidi huko kusini na katikati mwa Somalia Jumamosi jioni na mapema jana Jumapili.

Wanachama wa al-Shabaab

Mapema mwezi huu, Jeshi la Taifa la Somalia lilitangaza kuwa limefanikiwa kuua wanachama 37 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab katika mji wa Hudur, eneo la Bakol huko kusini mwa nchi.

Kundi la kigaidi a kitakfiri la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaidah limehusika na mashambulizi mengi ndani ya Somalia na katika nchi jirani tokea mwaka 2007.