Misri yakosoa tena misimamo ya Ethiopia kuhusu Bwawa la Renaissance
(last modified Wed, 01 Jul 2020 06:39:03 GMT )
Jul 01, 2020 06:39 UTC
  • Sameh Shoukry
    Sameh Shoukry

Serikali ya Misri imekosoa utendaji na mienendo ya Ethiopia kuhusiana na ujenzi wa Bwawa la Renaissance (al Nahdha) juu ya Mto Nile lakini imeeleza kwamba, ina matumaini na matokeo ya mazungumzo yaliyopangwa kusimamiwa na Umoja wa Afrika kujadili kadhia hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Sameh Shoukry ameituhumu Ethiopia kwamba imekataa kutoa taarifa sahihi kwa kamati za masuala ya ufundi kuhusiana na ujenzi wa Bwawa la Renaissance na usalama wake katika kipindi chote cha mazungumzo na kwamba kwa sababu hiyo Sudan ina wasiwasi kuhusu usalama wa bwawa linalojengwa umbali wa kilomita 20 kutoka kwenye mpaka wake, kwani kiwango kikubwa cha maji yanayozuiwa katika bwawa hilo kinaweza kuwa hatari kubwa kwa nchi hiyo. 

Sameh Shoukry amesema Misri inasubiri kuambia wakati wa mazungumzo hayo na nani atayasimamia, japokuwa inawezekana kwamba, nchi ya Afrika Kusini ambayo ndiye Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika, itachukua jukumu hilo.

Ujenzi wa Bwawa la Renaissance unaofanyika nchini Ethiopia juu ya maji ya Mto Nile umezusha mgogoro mkubwa baina ya nchi hiyo na nchi za Misri na Sudan. 

Misri na Sudan zina wasiwasi kwamba, ujenzi wa Bwawa la Renaissance na kuanza kufanya kazi bwawa hilo kutapunguza mgao wa maji wa nchi hizo. Misri inatambua ujenzi wa bwawa hilo kuwa ni tishio kwa usalama wake wa kitaifa kwa sababu karibu asilimia 90 ya mahitaji yake ya maji yanadhaminiwa kutokana na Mto Nile.

Ethiopia inakanusha madai hayo ikisema Bwawa la Renaissance ni muhimu sana kwa ajili ya ustawi wa maendeleo ya taifa hilo.

Tags