Uturuki: Ufaransa imefumbia macho jinai zinazofanywa na UAE, Misri nchini Libya
(last modified Thu, 02 Jul 2020 02:15:10 GMT )
Jul 02, 2020 02:15 UTC
  • Uturuki: Ufaransa imefumbia macho jinai zinazofanywa na UAE, Misri nchini Libya

Balozi wa Uturuki mjini Paris ameituhumu Ufaransa kuwa inaegemea upande mmoja na kwamba imefumbia macho jinai zinazofanywa na Umoja wa Falme za Kiarabu na Misri nchini Libya.

Ismail Hakki Musa alisema hayo jana Jumatano mbele ya kikao cha maseneta wa Ufaransa na kufafanua kuwa, "wakati unapounga mkono serikali halali, unatuhumiwa kuwa unacheza mchezo hatari, lakini wakati nchi kama UAE na Misri zinapomuunga mkono Haftar zinaonekana zimechukua hatua halali na huo hautizamwi kama mchezo hatari. Huko nitakuita kuegemea upande mmoja."

Matamshi hayo ya mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Uturuki ni radiamali kwa kauli ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ambaye Jumatatu iliyopita alikutana na Rais Kais Saied wa Tunisia mjini Paris na kusema: "Harakati za Uturuki nchini Libya ni jinai za kivita zinazohatarisha maslahi ya Ufaransa, nchi jirani na Umoja wa Ulaya."

Balozi wa Uturuki mjini Paris amekosoa vikali undumakuwili wa Ufaransa kwa kufumbia macho ukiukaji wa vikwazo vya silaha dhidi ya Libya unaofanywa na baadhi ya nchi na kubainisha kuwa, kila siku ndege za Imarati zinawapelekea silaha wapiganaji wa jenerali muasi wa Libya, Khalifa Haftar.

UN inataka mgogoro wa Libya upitiwe ufumbuzi wa kisiasa 

Hii ni katika hali ambayo, Stephanie Williams, Naibu Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya amekosoa upuuzaji wa mataifa mbalimbali kuhusu vikwazo vya silaha vya umoja huo dhidi ya Libya na kusema: Vikwazo vya silaha dhidi ya Libya vimekuwa vikikiukwa kuanzia ardhini, angani na hata baharini. Kuna haja ya suala hili kufuatiliwa na wahusika kuchukuliwa hatua.

Mbali na Ufaransa, genge hilo la wanamgambo linalojiita Jeshi la Taifa la Libya linasaidiwa kwa hali na mali na nchi kama Saudi Arabia, Misri, Ufaransa na Imarati. Hitilafu na mivutano baina ya Ufaransa na Uturuki zimepamba moto katika kipindi hiki ambacho nchi kadhaa zimejitumbukiza katika mgogoro wa ndani wa Libya. 

Tags