Misri yawasiliana na mtoto wa Gaddafi ili kujinufaisha kiuchumi nchini Libya
(last modified Sat, 04 Jul 2020 11:50:46 GMT )
Jul 04, 2020 11:50 UTC
  • Misri yawasiliana na mtoto wa Gaddafi ili kujinufaisha kiuchumi nchini Libya

Baadhi ya duru za Misri zimesema kuwa, mashirika ya kijasusi ya nchi hiyo yamewasiliana na mwana wa kiongozi wa zamani wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi kwa ajili ya kumshinikiza kisiasa na kujinufaisha na fursa za kiuchumi nchini humo.

Mtandao wa al Arabi al Jadid umezinukuu baadhi ya duru za ndani ya Misri zikifichua kuwa, baada ya Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa kupata ushindi mkubwa katika wiki za hivi karibuni dhidi ya jenerali muasi Khalifa Haftar ambaye mwezi Aprili mwaka jana 2019 alianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya mji mkuu wa Libya Tripoli kwa tamaa ya kuiangusha Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa inayotambuliwa na jamii ya kimataifa, sasa maafisa wa mashirika ya kijasusi ya Misri wameamua kumtafuta na kuwasiliana na Seif al Islam, mwana wa kiume wa Kanali Muammar Gaddafi ili kujinufaisha kiuchumi.

Duru hizo zimesema kuwa, mgogoro wa kiusalama na kisiasa baina ya Misri na Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya umezidi kuwa mkubwa baada ya Cairo kutafuta njia za kujinufaisha kiuchumi na mgogoro wa Libya.

Jenerali muasi, Khalifa Haftar

 

Kwa mujibu wa mtandao wa al Arabi al Jadid, kuwatafutia fursa za kazi raia wa Misri suala ambalo litasaidia katika juhudi za kukuza uchumi wa Misri, ni miongoni mwa malengo makuu ya serikali ya Cairo. Itakumbukwa kuwa Misri ni mmoja wa waungaji mkono wakuu wa jenerali muasi, Khalifa Haftar anayeongoza wanamgambo wanaojiita "Jeshi la Taifa la Libya."

Hivi karibuni, Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya ilifanikiwa kuwafurusha wanamgambo wa Haftar katika maeneo yote ya viunga vya mji mkuu Tripoli waliyokuwa wameyateka baada ya kuanzisha mashambulio ya pande zote dhidi ya mji huo mwezi Aprili 2019.

Tags