Wanajeshi 23 wa Nigeria wauawa katika shambulio la Boko Haram
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i62091-wanajeshi_23_wa_nigeria_wauawa_katika_shambulio_la_boko_haram
Maafisa usalama nchini Nigeria wametangaza kuwa, wanajeshi 23 wa nchi hiyo wameuawa kufuatia shambulio la kundi la kigaidi la Boko Haram katika mji wa Maiduguri wa kaskazini madhariki mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 09, 2020 03:09 UTC
  • Wanajeshi 23 wa Nigeria  wauawa katika shambulio la Boko Haram

Maafisa usalama nchini Nigeria wametangaza kuwa, wanajeshi 23 wa nchi hiyo wameuawa kufuatia shambulio la kundi la kigaidi la Boko Haram katika mji wa Maiduguri wa kaskazini madhariki mwa nchi hiyo.

Taarifa ya jeshi la Nigeria imeeleza pia kuwa, wanajeshi wengine wawili wamejeruhiwa huku wengine kadhaa wakiwa hawajulikani walipo. Wanajeshi hao walishambuliwa wakati walipokuwa katika doria na operesheni yao kuwasaka wanachama wa kundi hilo la kigaidi katika moja ya barabara kuu za mji wa Maiduguri.

Kwa mujibu wa jeshi la Nigeria wanachama 17 wa kundi la kigaidi la Boko Haram wameuawa pia katika mapigano yaliyozuka baada ya shambuulio la magaidi hao.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni jeshi la Nigeria lilitangaza habari ya kuuawa wanachama 75 wa kundi la kigaidi la Boko Haram katika operesheni 17 zilizofanyika baina ya Juni Mosi na Juni 30 mwaka huu.

Wanachama wa kunbdi la kigaidi la Boko Haram nchini Nigeria

Kwa zaidi ya muongo mmoja sasa ambapo, eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria limekuwa uwanja wa mashambulizi ya wanachama wa kundi la kigaidi Boko Haram ambao mwaka 2014 waliteka nyara mamia ya wasichana katika shule moja ya sekondari mjini Chibok.

Zaidi ya watu elfu 30 wameuawa na wengine wanaokaribia milioni tatu wamelazimishwa kuwa wakimbizi kutokana na mashambulizi ya kundi hilo la Boko Haram nchini Nigeria tokea mwaka 2009.

Kundi la Boko Haram ambalo maana yake ni "Elimu za Magharibi ni Haramu" ni genge la kigaidi na ukufurishaji lenye mitazamo potofu kuhusu mafundisho matukufu ya Uislamu na limekuwa likifanya jinai na ukatili mkubwa kwa watu wa kawaida hata Waislamu.