Misri yataka nchi za dunia ziache kupeleka magaidi maeneo ya machafuko
Mwakilishi wa kudumu wa Misri katika Umoja wa Mataifa ametoa mwito kwa viongozi wa baadhi ya nchi waache kupeleka magaidi katika maeneo ya machafuko hasa wakati huu wa kuenea maambukizi ya kirusi cha corona.
Televisheni ya Rusia al Yaum imemnukuu Mohamed Edrees akisema hayo katika kikao cha kufunga shughuli za Wiki ya Mawasiliano ya Intaneti kwa ajili ya kupambana na ugaidi zilizoendeshwa chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa, wakati umefika kwa baadhi ya nchi kuacha vitendo vyao visivyo sahihi vya kupeleka magaidi wa kigeni katika maeneo ya machafuko tena wakati huu ambao dunia nzima imekumbwa na ugonjwa wa COVID-19.
Mwakilishi huyo wa kudumu wa Misri katika Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, maambukizi ya kirusi cha corona yanalifanya kuwa jambo la dharura kuongeza jitihada za kimataifa za kukabiliana na ugaidi wa aina zote kama vile ugaidi wa kibiolojia, ugaidi wa mawasiliano ya kompyuta na pia matamshi na fikra za kibaguzi na misimamo mikali.
Vile vile amesema, mchakato wa kuchunguza mkakati wa kukabiliana na ugaidi kwa usimamizi wa Umoja wa Mataifa ambao umeakhirishwa hadi mwakani, ni fursa nzuri ya kutilia mkazo upya ahadi za kisiasa za nchi wanachama wa umoja huo kwa ajili ya kukabiliana vilivyo na vitisho vya ugaidi kimataifa.