Kuafiki bunge la Misri jeshi la nchi hiyo lipelekwe Libya
Wakati mgogoro na mapigano yangali yanaendelea nchini Libya, uingiliaji wa madola ajinabi katika masuala ya ndani ya nchi hiyo umezidi kuongezeka. Katika mwendelezo wa uingiliaji huo, siku ya Jumatatu bunge la Misri lilitoa idhini kwa rais Abdel Fattah el Sisi ya kutuma askari na kujiingiza kijeshi nchini Libya itapolazimu kufanya hivyo; na vilevile likaafikiana na mpango wa kutumwa vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo nje ya nchi kwa ajili ya shughuli za kijeshi.
Vita nchini Libya vimezidi kupamba moto; na nchi hiyo si uwanja wa vita baina ya vikosi vinavyounga mkono Serikali ya Muafaka wa Kitaifa (GNA) na askari wanaoongozwa na jenerali mwasi Khalifa Haftar peke yao, lakini hivi sasa vikosi vya kigeni navyo pia vinaonekana wazi wazi katika uga wa siasa na medani za mapigano na vita za nchi hiyo. Misri, Imarati na Saudi Arabia ni waungaji mkono wakuu wa kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya (LNA) linaloongozwa na Khalifa Haftar katika sarakasi ya siasa za Libya, huku Uturuki nayo ikiwa ni muungaji mkono mkuu wa Serikali ya Muafaka wa Kitaifa.
Katika miezi ya karibuni, kwa msaada na uungaji mkono wa wangamgambo wenye mfungamano na Uturuki, Serikali ya Muafaka wa Kitaifa ya Libya imepata mafanikio makubwa ya kuyakomboa maeneo mbali mbali ya nchi hiyo na kuwatimua wapiganaji wa kundi la LNA, mpaka ikafika hadi maafisa wa serikali hiyo kusikika wakizungumzia kukaribia kupata ushindi mkubwa na kukataa mipango iliyopendekezwa kwa ajili ya kusitisha vita na kuanzisha mazungumzo ya kutafuta mwafaka wa kufikia suluhu ya mgogoro wa nchi hiyo. Miongoni mwa mipango muhimu zaidi iliyopendekezwa, ni ule uliowasilishwa na Misri ambao pamoja na mambo mengine, umependekeza kusitishwa mapigano nchini Libya, kuanza tena mazungumzo ya suluhu mjini Geneva, Uswisi kwa usimamizi wa Umoja wa Mataifa, kuvunjwa makundi ya wanamgambo, kukabidhiwa silaha kwa jeshi la taifa la Libya, kuondolewa mamluki wa kigeni walioko nchini humo na kuendelea mazungumzo baina ya Walibya wenyewe katika kalibu ya 5+5 kwa usimamizi wa Umoja wa Mataifa.
Katika jibu alilotoa kwa pendekezo la usitishaji vita lililotolewa na Misri na Khalifa Haftar, Muhammad Qanunu, msemaji rasmi wa jeshi la Serikali ya Muafaka wa Kitaifa alisema: Serikali hiyo haina muda wa kupoteza; na vikosi vya jeshi la Libya vitaendeleza kwa nguvu na uwezo kamili operesheni za kuwaandama wanamgambo magaidi wa Haftar.
Baada ya ushindi kadhaa viliopata vikosi vya serikali ya Muafaka wa Kitaifa katika maeneo ya kusini mwa mji mkuu Tripoli na mji wa Tarhuna mwanzoni mwa mwezi uliopita wa Juni, vikosi hivyo vilitangaza pia kuwa vinasonga mbele kuelekea mji wa Sirte kwa lengo la kuukomboa mji huo na kituo cha anga cha Al-Jufra. Hata hivyo kusonga mbele kuelekea Sirte kunatafsiriwa kama kengele ya hatari kubwa kwa Msiri, kiasi kwamba rais wa nchi hiyo Abdel Fattah el Sisi alionya juu ya hatua hiyo na ya kukitwaa kituo cha anga cha Al-Jufra akisisitiza kuwa huo ni mstari mwekundu kwa nchi yake. Viongozi wa Misri wanadai kuwa, harakati za serikali ya Muafaka wa Kitaifa na hasa katika mji wa Sirte zinaweza kuhatarisha usalama wa mpakani mwa Misri na hasa kushamirisha uwepo wa makundi ya kigaidi.
Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri amesema: Hatutafunga mikono tu kuhusiana na matukio ya mji wa Sirte ambayo yanaweza kuhatarisha usalama wa taifa wa Misri na Libya na tunaweza kuibadilisha haraka na kwa nguvu hali ya kijeshi ya nchi hiyo.
Misri imetoa kitisho hicho katika hali ambayo viongozi wa Serikali ya Muafaka wa Kitaifa ya Libya walikwisha tahadharisha hapo kabla kuhusu hatua za Misri za kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo. Kwa mtazamo wa viongozi wa GNA Misri ni msababishaji wa kushadidi hitilafu na kuendelea vita nchini Libya.
Muhammad al-Qablawi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Serikali ya Muafaka wa Kitaifa ya Libya amesema: Rais wa Misri ametangaza kuwa lengo lake ni kuleta suluhu lakini ni mchocheaji mapigano na vita nchini Libya.
Kutokana na uamuzi uliotangazwa na Misri, safu za makabiliano ya kisiasa nchini Libya zimebadilika; na hali ya mambo imekuwa tata zaidi. Ukweli ni kwamba, Libya imegeuzwa kuwa uwanja wa vita vya niaba vya nchi zinazoingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo zikiongozwa na Uturuki na Misri. Nchi hizo mbili, ambazo zenyewe zinaungwa mkono na baadhi ya nchi za eneo na za Magharibi zinafanya juu chini kuhakikisha zinaibuka washindi katika vita vya Libya ili kwa kutumia satua na ushawishi wao si tu ziweze kufaidika na maliasili na utajiri wa nchi hiyo wao na waitifaki wao, lakini pia kwa kuitumia Libya kama lango la kuingilia Afrika, ziweze kupanua satua na ushawishi wao barani humo.
Siku zijazo zitakuwa ni siku muhimu sana za kuamua hatima ya mustakabali wa kisiasa wa Libya. Inavyoonekana, endapo Misri itajiingiza kijeshi Libya, Uturuki nayo itajizatiti zaidi kijeshi na kuitumbukiza nchi hiyo katika vita kamili na vya pande zote. Pamoja na hayo juhudi na hatua za mashauriano kwa ajili kuhakikisha vita vinasimamishwa nchini Libya zingali zinaendelea.../