Misri yatoa vitisho dhidi ya Ethiopia kuhusiana na Bwawa la al-Nahdha
Mjumbe wa timu ya Misri katika mazungumzo kuhusu Bwawa la al-Nahdha ametishia kuwa, endapo hakutafikiwa mwafaka katika kadhia hiyo, serikali ya Cairo itachukua hatua ya upande mmoja dhidi ya Ethiopia.
Alaa Al-Zawahiri sambamba na kuashiria kuwa Misri ina machaguo mengi ya kuyajadili ametishia kuwa, kama hadi kufikia Oktoba mwaka huu wa 2020 kutakuwa hakujafikiwa makubaliano baina yake na Sudan na Ethiopia kuhusiana na ujazaji maji na kuanza kutumika bwawa hilo, Cairo italazimika kuchukua hatua ya upande mmoja.
Mjumbe wa timu ya Misri katika mazungumzo kuhusu Bwawa la al-Nahdha amedai kuwa, ujazaji maji wa bwawa hilo ni tishio kwa amani na usalama wa kimataifa na kuongeza kwamba, hatua ya Ethiopia ya kuchukua hatua maalumu katika uwanja wa kujaza maji katika Bwawa la al-Nahdha inalenga kuilazimisha Cairo ijitoe katika mazungumzo hayo na hivyo iituhumu kwamba, haina nia ya kupatiwa ufumbuzi kadhia hiyo kupitia njia za amani.
Nchi tatu za Kiafrika za Misri, Sudan na Ethiopia zinahitalifiana kuhusu haki ya kila nchi kwa Mto Nile na namna ya kugawana maji ya mto huo. Hata hivyo juhudi mbalimbali za kutatua hitilafu za nchi hizo tatu zimegonga mwamba hadi sasa.
Ethiopia ilianza kujenga Bwawa la An Nahdhah mwanzoni mwa mwaka 2011 hata hivyo hitilafu kali baina yake na Misri na Sudan zimepelekea kuakhirishwa mchakato wa ujenzi na kutumiwa maji ya mto huo.