Rais Sisi wa Misri aidhinisha sheria ya kuwazuia wanajeshi kuwania urais
Rais Abdul Fattah al-Sisi wa Misri ameidhinisha sheria ya kupiga marufuku wanajeshi walio kazini na waliostaafu kuwania urais au ubunge bila idhini ya jeshi.
Sheria hiyo mpya inakuja baada ya Wamisri kupiga kura mwaka jana kuidhinisha mabadiliko ya katiba ambayo yatamuwezesha al-Sisi, ambaye ni jenerali wa zamani jeshini, kubakia madarakani hadi mwka 2030.
Sheria mpya iliyopitishwa Jumatano itafanya iwe viumu sana kwa maafisha wa kijeshi kugombea kiti chochote cha kisiasa na kwa msingi huo kuwazuia wapinzani wenye nguvu kuibuka dhidi ya al-Sisi.
Tokea Misri iwe jamhuri ya kisasa, marais wake wote isipokuwa wawili walikuwa ni wanajeshi.
Al-Sisi aliongoza mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa Muhammad Morsi madarakani mwaka 2013. Morsi, ambaye alifariki dunia akiwa gerezani, alikuwa rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia Misri.
Mkuu wa zamani wa majeshi ya Misri, Sami Anan, alifungwa jela Januari 2018 baada ya kujitokeza kugombea urais dhidi ya al-Sisis bila idhini ya jeshi. Aliachiliwa huru miaka miwili baadaye.