Sudan yakataa pendekezo la Ethiopia kuhusu Bwawa la al-Nahdha
(last modified Thu, 06 Aug 2020 04:30:33 GMT )
Aug 06, 2020 04:30 UTC
  • Sudan yakataa pendekezo la Ethiopia kuhusu Bwawa la al-Nahdha

Wizara ya Umwagiliaji ya Sudan imesema, nchi hiyo haijakubali pendekezo la Ethiopia kuhusu kujaza maji na kutumia Bwawa la al-Nahdha (GERD).

Taarifa iliyotolewa na Wizara hiyo imesema, Sudan imekataa pendekezo la Ethiopia kwa kuwa linaelekeza kuwa, makubaliano yanapaswa kuhusisha awamu ya kwanza tu ya kujazwa  maji bwawa hilo.

Kutokana na taarifa hiyo, Sudan inachukulia pendekezo hilo kama kubadilika kwa msimamo wa Ethiopia, ambao unatishia mwendelezo wa mazungumzo ya pande tatu kati ya Sudan, Misri na Ethiopia.

Masharti ya awali ya Sudan kushiriki katika mazungumzo ya bwawa la Mto Nile ni kwamba makubaliano ya kujaza maji na kutumiwa bwawa la GERD hayapaswi kuunganishwa na kufikia mkataba kuhusu maji ya Blue Nile.

Hayo yanajiri wakati ambao Misri nayo imetangaza kusitisha mazungumzo yake na Ethiopia kuhusiana na kadhia ya bwawa hilo la al-Nahdha kutokana na kile ilichokieleza kuwa, hatua ya upande mmoja ya Addis Ababa ya kuanza kujaza maji katika bwawa hilo.

Ujenzi wa Bwawa la al-Nahdha unaofanywa na Ethiopia juu ya maji ya Mto Nile tangu mwaka 2011 umezusha mvutano mkubwa baina ya nchi tatu za Misri, Sudan na Ethiopia.

Misri na Sudan zina wasiwasi kwamba ujenzi wa bwawa hilo utapunguza mgao wao wa maji na kusababisha tatizo kubwa la maji katika nchi hizo. Hadi sasa kumefanyika duru kadhaa za mazungumzo baina ya wawakilishi wa nchi hizo tatu lakini hayajakuwa na matokeo ya kuridhisha.

Tags