Bobi Wine asema Polisi Uganda wamefyatua risasi kuwatawanya wafuasi wake
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i62702-bobi_wine_asema_polisi_uganda_wamefyatua_risasi_kuwatawanya_wafuasi_wake
Bobi Wine, nyota wa muziki na mwanasiasa machachari anayetazamiwa kuwania urais katika uchaguzi mkuu unaotazamiwa kufanyika mwaka ujao nchini Uganda amesema baadhi ya wafuasi wake walijeruhiwa hapo jana baada ya polisi kufyatua risasi na mabomu ya kutoa machozi kutawanya umati wa watu huko mashariki mwa nchi hiyo.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Aug 09, 2020 03:27 UTC
  • Bobi Wine asema Polisi Uganda wamefyatua risasi kuwatawanya wafuasi wake

Bobi Wine, nyota wa muziki na mwanasiasa machachari anayetazamiwa kuwania urais katika uchaguzi mkuu unaotazamiwa kufanyika mwaka ujao nchini Uganda amesema baadhi ya wafuasi wake walijeruhiwa hapo jana baada ya polisi kufyatua risasi na mabomu ya kutoa machozi kutawanya umati wa watu huko mashariki mwa nchi hiyo.

Wine, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, anapigania kuhitimisha utawala wa miaka 34 wa Rais Yoweri Kaguta Museveni katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mapema 2021.

Kupitia ujumbe alioandika kwenye ukurasa wake wa Facebook, mwanasiasa huyo amesema, alikuwa ameelekea mjini Mbale mashariki mwa nchi kwa ajili ya kushiriki katika kipindi maalumu cha mazungumzo redioni lakini maafisa wa usalama wa polisi na jeshi walimzuia. 

Bobi Wine amefafanua katika ujumbe wake huo kwamba: "Baada ya hapo askari polisi walianza kufyatua mabomu ya kutoa machozi na risasi moto. Makomredi wengi walijeruhiwa na sasa wanatibu majeraha". Hata hivyo Wine hakutaja idadi halisi ya waliojeruhiwa.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda

Robert Kyagulanyi ambaye kitasnia ni mwanamuziki, alijiunga na siasa za Uganda mwaka 2017 baada ya kushinda ubunge kupitia uchaguzi mdogo na hatimaye akatangaza nia yake ya kugombea urais.

Uamuzi wake huo umevutia uungaji mkono mkubwa hususan miongoni mwa vijana nchini humo wanaovutiwa na muziki wake wenye jumbe za kisiasa za kulalamikia ukiukaji mkubwa wa haki za watu, ufisadi na utawala wa muda mrefu wa Rais Museveni.

Mbali na wafuasi wake, Bobi Wine mwenyewe alipigwa na kujeruhiwa vibaya na askari wa usalama wa Uganda mwaka 2018  na kulazimika kusafiri kwenda Marekani kwa ajili ya matibabu.

Mwezi uliopita chama tawala nchini Uganda NRM kilipitisha Rais Museveni kuwa mgombea wake wa urais katika uchaguzi ujao. Endapo atashinda kwa muhula mwingine, Museveni anaweza kurefusha utawala wake na kutimiza miaka 40 na kuwa mmoja wa viongozi waliodumu kwa muda mrefu zaidi madarakani barani Afrika.../