Makaburi mawili ya umati yapatikana kandokando ya mji mkuu wa Rwanda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i62889-makaburi_mawili_ya_umati_yapatikana_kandokando_ya_mji_mkuu_wa_rwanda
Mabaki ya makumi ya miili ya wahanga wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda dhidi ya Watutsi yamepatikana katika wilaya ya Nyarugenge kandokando ya mji mkuu wa Rwanda, Kigali.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 18, 2020 14:57 UTC
  • Makaburi mawili ya umati yapatikana kandokando ya mji mkuu wa Rwanda

Mabaki ya makumi ya miili ya wahanga wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda dhidi ya Watutsi yamepatikana katika wilaya ya Nyarugenge kandokando ya mji mkuu wa Rwanda, Kigali.

Taarifa zinasema makaburi hayo mawili ya umati yamepatikana katika nyumba ya mwanachama wa zamani wa wanamgambo wa Interahamwe, ambao walihusika pakubwa na mauaji ya kimbari ya Rwanda.

Kwa mujibu wa Masengo Rutayisire, mkuu wa IBUKA,  ambayo ni jumuiya ya manusura wa mauaji ya kimbari katika wilaya hiyo, hadi sasa zaidi ya mabaki ya watu 100 yamepatikana.

Mabaki ya waliouawa katika mauaji ya kimbari Rwanda

Amesema miili hiyo ni ya wale waliouawa katika kituo cha upekuzi barabarani ambacho kilikuwa katika eneo hilo kilichokuwa kikisimamiwa na mwanachama wa Interahamwe, Francois Simbizi, mita chache kutoka nyumba yake.

Simbizi alipatikana na hatia ya kuhusika na mauaji ya kimbari na alifariki dunia akitumikia kifungo chake gerezani.

Miili ya waliouawa katika mauaji ya kimbari ya Rwanda hupatikana mara kwa mara katika maeneno mbalimbali ya nchi hiyo kutokana na ukosefu wa taarifa kuhusu walikozikwa kwa umati. Kwa mujibu wa ripoti ya Tume ya Taifa ya Kupambana na Mauaji ya Kimbari ya Rwanda, mabaki watu 118,049 ya wahanga wa mauaji ya kimbari ilipatikana baina ya 2018 na 2019.

Karibu watu milioni moja, wengi wao wakiwa wa kabila la Tutsi, waliuawa katika mauaji ya kimbari ya Rwanda yaliyofanywa na Wahutu wenye misimamo mikali mwaka 1994.