Wavuvi Wairani waliokuwa wanashikiliwa mateka na maharamia Somalia waachiliwa huru
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetangaza kuwa, kundi la mwisho la mabaharia Wairani ambao walitekwa nyara na maharamia wa Somalia mwaka 2015 hatimaye wameachiliwa huru.
Siku ya Alhamisi Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran ilitangaza kuwa, raia watatu Wairani ambao walikuwa wanashikiliwa mateka Somalia waliachiliwa huru katika oparesheni ya maafisa usalama wa Iran kwa ushirikiano wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran na Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).
Katika taarifa siku ya Ijumaa, Waliullah Mohammadi, Mkurugenzi wa Kitengo cha Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alisema: 'Miongoni mwa mabaharia 37 Wairani waliotekwa nyara mwaka 2015, hawa wavuvi walikuwa kundi la mwisho kuachiliwa huru."
Mohammadi amesema kuwa hapo kabla makundi mawili ya mabaharia Wairani walifanikiwa kutoroka wakiwa wanashikiliwa na maharamia wa Somalia na kurejea Iran. Ameongeza kuwa makundi mengine mawili ya mateka Wairani waliachiliwa huru na kurejea nyumbani kutokana na jitihada za idara kadhaa za Iran na Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran.