Mvua na mafuriko yaua watu 45 nchini Niger
(last modified Sat, 29 Aug 2020 23:55:05 GMT )
Aug 29, 2020 23:55 UTC
  • Mvua na mafuriko yaua watu 45 nchini Niger

Kwa akali watu 45 wameaga dunia kufuatia mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazonyesha nchini Niger.

Aidha watu zaidi ya 226,000 wamelazimika kuyahama makazi yao katika kipindi cha wiki moja iliyopita, kutokana na mafuriko hayo hususan eneo la Magharibi mwa nchi.

Mvua hizo zimesababisha Mto Niger kujaa hadi pomoni na kuvunja kingo zake, jambo ambalo limevuruga shughuli za uchukuzi na mawasiliano katika mji mkuu Niamey.

Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Brigi Rafini ambaye ameyatembelea maeneo na familia zilizoathirika na majanga hayo ya kimaumbile amesema, "nilidhani mji mkuu Niamey umesalimika na mafuriko. Kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, hakuna aliyesalimika na mafuriko."

Ramani ya Niger

Baraza la Mawaziri limetangaza kuwa, nyumba 25,800 zimeathiriwa moja kwa moja na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa inayonyesha nchini humo tokea Jumatatu iliyopita.

Mbali na kusomba mashamba ya kilimo, mafuriko hayo yamebomoa madarasa 64 na misikiti 24 katika maeneo mbali mbali ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

 

Tags