Sep 05, 2020 02:33 UTC
  • Sudan na kundi kuu la waasi zakubaliana kuanzisha tena mazungumzo ya amani

Serikali ya Sudan na kundi kuu la waasi linaloendesha harakati zake katika maeneo ya mpakani ya kusini mwa nchi hiyo zimeafikiana kuanzisha tena mazungumzo amani chini ya uwenyeji wa Sudan Kusini.

Serikali ya Sudan imekubaliana na Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Sudan upande wa kaskazini inayoongozwa na Abdelaziz al Hilli; moja ya makundi ambayo halikuwepo wakati wa utiaji saini wa makubaliano ya amani uliofanyika Jumatatu iliyopita.

Waziri Mkuu wa Sudan, Abdallah Hamdok

Harakati hiyo inayoongozwa na Abdelaziz al Hilli imekubaliana na serikali ya Khartoum juu ya umuhimu wa kutafutwa suluhisho kamili la kisiasa huko Sudan na kutatua vyanzo vya mzozo nchini humo. Hayo yameelezwa jana Ijumaa na ofisi ya Waziri Mkuu wa Sudan, Abdallah Hamdok.

Aman Amum, mpatanishi mkuu wa harakati hiyo ya ukombozi ya watu wa Sudan upande wa kaskazini amesema kuwa, ni kweli wamefikia mapatano na serikali ya Sudan, na mazungumzo yamefanyika huko Addis Ababa kati yao na Waziri Mkuu wa Sudan Hamdok. Amesema wataendelea kufanya mazungumzo chini ya upatanishi wa serikali ya Juba.

Tags