Al-Shabaab yadai kuua watu 16 Somalia wakiwemo askari wa Marekani
Wanamgambo wa al-Shabaab wametangaza kuhusika na mripuko wa bomu ulioua watu 16, wakiwemo wanajeshi wanne wa Kamandi ya Jeshi la Marekani Afrika (AFRICOM).
Taarifa iliyotolewa na kundi hilo la kigaidi na kitakfiri imedai kuwa, watu 12 wamejeruhiwa katika shambulizi hilo la jana Jumatatu katika eneo la Janay Abdalle, yapata kilomita 50 magharibi mwa Kismayo, makao makuu ya muda ya eneo la Jubaland.
Kamandi ya Jeshi la Marekani Afrika ina askari zaidi ya 600 katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. na baadhi yao wapo katika kambi ya kijeshi ya Janay Abdalle eneo la Jubaland.
Hiyo jana, Mohamed Ahmed Sabriye, mkurugenzi wa mawasiliano wa jimbo la Jubaland aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa, wanajeshi wawili wa kikosi maalumu cha Somalia wameuawa na afisa mmoja wa jeshi la Marekani amejeruhiwa katika mripuko wa bomu uliotokea nje ya kambi ya kijeshi ya kusini mwa nchi hiyo.
Licha ya kuwepo mamia ya askari wa Marekani na maelfu ya wanajeshi wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (Amisom), lakini nchi hiyo ya Pembe ya Afrika inaendelea kushuhudia wimbi la mashambulizi ya kundi la al-Shabaab kwa miaka mingi sasa.
Tangu mwaka 2007, kundi la ukufurishaji la al Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida limekuwa likifanya mashambulizi ndani na nje ya Somalia kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya nchi hiyo.