Russia: Tuko tayari kuongeza idadi ya washauri wa kijeshi CAR
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ambaye pia ni mjumbe maalumu wa Rais Vladimir Putin wa Russia katika masuala ya Asia Magharibi na Afrika amesema kuwa, Moscow iko tayari kuongeza idadi ya washauri wake wa kijeshi huko Jamhuri ya Afrika ya Kati iwapo kutaonekana kuna udharura wa kufanya hivyo.
Mikhail Bogdanov amesema hayo mwishoni mwa kikao cha pamoja cha Russia na bara la Afrika ikiwemo pia jumuiya ya ushirikiano wa kiuchumi ya Afrika ameongeza kwambs, kama kutakuwa na udharura wa kutuma washauri zaidi wa kijeshi huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, basi Moscow iko tayari kkufanya hivyo.
Mwanzoni mwa mwaka 2018, Russia ilituma walimu watano wanajeshi na walimu 170 wasio wanajeshi kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa maafisa wa kijeshi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati katika masuala mbalimbali ya kijeshi na kijamii.
Mwaka 2013, Jamhuri ya Afrika ya Kati ilikumbwa na machafuko makubwa ya ndani. Machafuko hayo yalitokea baada ya kuondolewa madarakani rais wa zamani wa nchi hiyo François Bozizé kufuatia hujuma ya waasi wa Seleka.
Tangu wakati huo hadi sasa nchi hiyo imekuwa uwanja wa mapigano ya kila uchao kati ya makundi hasimu, hususan lile la Kikristo la Anti-Balaka na kundi la Seleka. Magaidi wa kundi la Kikristo la Anti-Balaka wameua idadi kubwa ya Waislamu. Wakati huo Waislamu wengi waliuawa kwa umati na wengi kulazimika kuwa wakimbizi kufuatia hujuma za genge hilo la Kikristo la Anti-Balaka.