Mvua na mafuriko yaua na kujeruhi makumi nchini Burkina Faso
Serikali ya Burkina Faso imetangaza kuwa nchi hiyo inakabiliwa na janga la kimaumbile baada ya watu 13 kupoteza maisha kutokana na mafuriko, huku wengine 19 wakijeruhiwa.
Abdoul Karim Sango, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Utalii wa nchi hiyo amesema mafuriko hayo yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha kwa siku kadhaa sasa nchini humo yameathiri idadi kubwa ya watu.
Wizara ya Fedha ya Burkina Faso imetangaza kutenga dola milioni 9 kwa ajili ya waathiriwa wa mafuriko hayo hususan waliopoteza makazi yao.
Siaka Ouattara, mkazi wa kijiji cha Marabagasso kilichoko kusini magharibi mwa nchi ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, mawasiliano yamekatika baina ya kijiji hicho na mji wa Bobo Dioulasso, umbali wa kilomita 70 toka kijijini hapo, baada ya daraja lililokuwa limeyaunganisha maeneo hayo mawili kusombwa na mafuriko.

Duru za kiusalama zimeripoti kuwa, mafuriko hayo yameathiri pia operesheni za kukabiliana na magenge yenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda na genge la ISIS (Daesh).
Nchi kadhaa za Afrika zinashuhudia mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazonyesha kwa wiki kadhaa sasa. Jumamosi iliyopita serikali ya Sudan ilitangaza hali ya hatari nchini humo kutokana na mafuriko makubwa ambayo yameua zaidi ya watu mia moja na kuharibu zaidi ya nyumba laki moja.