Wanaobaka watoto wadogo jimboni Kaduna, Nigeria kuhasiwa
Wabunge katika jimbo la Kaduna nchini Nigeria wamepasisha muswada wa sheria inayotoa adhabu ya kuwahasi wale wataokutwa na hatia ya kuwabaka watoto walio chini ya umri wa miaka minne.
Gavana wa jimbo hilo, Nasir Ahmad el-Rufai anatakiwa kutia saini muswada huo ili kuwa sheria katika jimbo hilo la Kaskazini Magharibi mwa Nigeria. Awali alitangaza kuunga mkono adhabu hiyo ili kudhibiti vitendo vya ubakaji vilivyokithiri jimboni hapo.
Sheria nchini Nigeria inatoa adhabu ya kifungo cha miaka 14 na kifungo cha maisha jela kwa wanaopatikana na hatia ya kubakaji, lakini wabunge wanaweza kupasisha adhabu tofauti.
Unyanyapaa huwafaya waathirika kushindwa kuripoti matukio ya ubakaji nchini Nigeria; huku idadi ya watu waliofikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa kosa hilo ni ndogo.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, ubakaji unatumiwa na magaidi kama moja ya mbinu zao katika nchi za Kiafrika zinashohudiwa machafuko kama vile Nigeria,Somalia na Mali.
Aidha Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch (HRW) limewahi kutangaza kuwa, askari usalama wa Nigeria wanawabaka na kuwadhalilisha kijinsia wanawake na mabinti wanaokimbia mashambulizi ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram katika eneo lililoathiriwa na machafuko la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.