28 wauawa katika mripuko wa lori la mafuta Nigeria
Kwa akali watu 28 wamepoteza maisha katika mripuko wa lori la mafuta katika jimbo la Kogi, katikati mwa Nigeria.
Bisi Kazeem, msemaji wa Idara ya Usalama wa Barabarani nchini humo (FRSC) amesema watoto tisa ni miongoni mwa watu walioaga dunia katika ajali hiyo iliyotokea mkabala wa kituo cha kuuzia mafuta katika barabara kuu ya Lokoja-Zariagi.
Gavana wa jimbo hilo, Yahaya Bello amesema ajali hiyo iliyotokea mapema jana Jumatano, mbali na kusababisha maafa ya binadamu, lakini pia imeharibu idadi kubwa ya magari, majengo na vitu vingine vya thamani.
Miripuko ya malori na mabomba ya kusafirishia mafuta na gesi imekuwa ikiripotiwa mara kwa mara nchini Nigeria, taifa la Afrika magharibi lenye utajiri wa bidhaa hizo.
Mapema mwaka jana, makumi ya watu walipoteza maisha katika mripuko wa lori la mafuta katika eneo la Odukpani, jimboni Cross River kusini mashariki mwa Nigeria.
Kadhalika Machi mwaka huu, mripuko wa bomba la gesi uliotokea katika mji mkuu wa kibiashara wa Lagos nchini Nigeria ulipelekea watu 15 kuaga dunia na makumi ya wengine kujeruhiwa.