Magaidi wanane wauliwa katika operesheni ya mashambulio ya jeshi la Somalia
Duru za habari zimeripoti kuwa magaidi wasiopungua wanane wameuliwa katika operesheni ya mashambulio iliyofanywa na jeshi la Somalia kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu.
Kwa mujibu duru hizo operesheni hiyo ya jeshi imefanywa katika eneo la Ligo kaskazini magharibi mwa mji mkuu huo wa Somalia.
Imeelezwa kuwa magaidi wawili kati ya wanane walioangamizwa ni miongoni mwa vinara wa kundi la kigaidi la Ash-Shabaab.
Katika upande mwingine, askari mmoja wa vikosi vya usalama ameuawa na mmoja mwengine amejeruhiwa katika shambulio la kigaidi lililofanywa mjini Mogadishu.
Tangu mwaka 2007 kundi la kigaidi la Ash-Shaabab limekuwa likifanya operesheni za hujuma na mashambulio kwa lengo la kuiangusha serikali ya Somalia.
Mnamo mwaka 2011, kundi hilo lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda lilitimuliwa katika mji mkuu Mogadishu kwa juhudi za jeshi la nchi hiyo likishirikiana na vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika AMISOM, hata hivyo lingali linaendelea kudhibiti sehemu kubwa ya maeneo ya vijijini mwa Somalia.../