Oct 09, 2020 02:37 UTC
  • Somalia, Cuba zakanusha madai ya kuachiwa huru madaktari waliotekwa na al-Shabaab

Serikali za Somalia na Cuba zimekanusha madai ya kuachiwa huru madaktari wawili wa Cuba waliotekwa nyara na kundi la kigaidi la al-Shabaab mwaka jana nchini Kenya.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia, Ahmed Issa Awad na Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Cuba, Juan Antonio Palacious wameyataja madai hayo kama uvumi usiokua na msingi wowote. Hata hivyo serikali ya Somalia imesisitiza kuwa jitihada za kuhakikisha madaktari hao wanaachiwa huru zinaendelea.

Serikali za Mogadishu na Havana zimetoa taarifa hiyo baada ya gazeti la Daily Mail la Ungereza kuripoti kuwa, wanachama wa al-Shabaab ambao kwa muda wa mwaka mmoja wamewashikilia mateka madaktari hao nchini Somalia, wameamua kuwaachilia huru baada ya kufanya mazungumzo na serekali husika. 

Madaktari hao ambao ni Daktari Assel Herera Corea na Daktari Landy Rodriguez walitekwa nyara  Aprili 12 mwaka jana 2019 wakiwa wanaelekea katika eneo lao la kazi mjini Mandera kaskazini mashariki mwa Kenya.

Madaktari Assel Herera Corea na Landy Rodriguez waliotekwa

Mei mwaka jana, magaidi wa kundi la al-Shabaab walitangaza kuwa wanataka walipwe Shilingi milioni 150 au takribani dola milioni 1.5 kama kikomboleo ili kuwaachilia huru madaktari hao.

Madaktari hao waliotekwa nyara ni miongoni mwa madaktari 100 wanaohudumu nchini Kenya kwa mujibu wa mkataba baina ya serikali za Nairobi na Havana na wametumwa katika kaunti zote 47 za nchi hiyo.

Tags