Uamuzi wa Sudan wa kuondoa askari wake katika vita vya Yemen
(last modified Sun, 11 Oct 2020 07:09:13 GMT )
Oct 11, 2020 07:09 UTC
  • Uamuzi wa Sudan wa kuondoa askari wake katika vita vya Yemen

Katika hali ambayo Saudi Arabia inaendelea kupiga ngoma ya vita huko nchini Yemen, waitifaki wake katika muungano huo wa kijeshi hawako tayari tena kuvumilia siasa za kupenda vita za Riyadh na hivi sasa wamo mbioni kujiondoa katika muungano huo.

Omar Qamar al-Din, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Sudan sambamba na kueleza kwamba, wanajeshi wa nchi hiyo waliingia katika vita huko Yemen katika kipindi cha utawala wa Omar al-Bashir amesema, serikali ya mpito ya nch hiyo inafanya juhudi kuhakikisha kwamba, inawaondoa askari wake wanaoshiriki kwenye vita vya muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya Yemen.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Sudan anazungumzia suala la kuondolewa majeshi ya nchi hiyo huko Yemen katika hali ambayo,  wiki chache zilizopita kuliripotiwa habari ya kutumwa askari wa Sudan huko Yemen na hivyo Khartoum kuongeza ushiriki wake katika vita hivyo. Mtandao wa Habari wa Middle East Eye hivi karibuni ulizinukuu duru za Saudia na kuandika: Wanajeshi 1,018 wa Sudan tarehe 22 Septemba waliingia Saudia kwa boti na kisha kuvuka mpaka kupitia idara ya uhamiaji ya mji wa Jazan ulioko kusini mashariki mwa nchi hiyo na kuingia nchini Yemen, na kwa muktadha huo, Khartoum imeongeza ushiriki wake katika vita hivyo.

Omar Qamar al-Din, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Sudan

 

Kuhusiana na hilo, Omar Qamar al-Din, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Sudan amedai kuwa, kuingia katika vita si sawa na kujiondoa katika vita hivyo. Sisi katika zama za Omar al-Bashir tuliingia katika vita vya Yemen lakini sasa hivi tunafanya juhudi ili kujiondoa katika vita hivyo na akthari ya wanajeshi wetu wamesharejea nyumbani na waliobakia huko ni wachache sana.

Sudan ni miongoni mwa mataifa muhimu ambayo baada ya kujiunga kwake na muungano vamizi wa Saudia katika miaka ya hivi karibuni imetuma maelfu ya wanajeshi wake katika vita huko Yemen vinavyoongozwa na utawala wa Aal Saud. Kimsingi ni kuwa, Omar al-Bashir Rais wa Sudan aliyeondolewa madarakani alifanya juhudi za kutuma majeshi ya nchi yake na kuwa pamoja na Saudia katika vita vya Yemen ili anufaike na misaada ya Riyadh, na kwa msingi huo aendelee kuhifadhi nafasi yake ya uongozi, hatua ambayo hata wakati huo ililalamikiwa vikali na vyama vya siasa ndani ya nchi hiyo.

Licha ya Sudan kushuhudia matukio mengi na mabadiliko ya uongozi ambapo Omar al-Bashir ameondolewa madarakani, lakini wanajeshi wa nchi hiyo wameendelea kubakia katika muungano vamizi wa kijeshi huko Yemen. Ukweli wa mambo ni kuwa, serikali ya muda ya Sudan nayo ililitumia kwa mara nyingine suala la uwepo wa wanajeshi wa nchi hiyo huko Yemen kama kura ya turufu na wenzo wa kupata himaya na uungaji mkono wa Saudia na hivyo kupatiwa misaada ya kifedha pamoja na himaya ya kisiasa.

Omar Hassan al-Bashir, Rais wa zamani wa Sudan

 

Hii ni katika hali ambayo, akthari ya wanajeshi hao ni vijana walio chini ya umri wa miaka 17 na ndio wanaounda idadi kubwa ya wanajeshi vamizi waliouawa huko Yemen. Kwa mujibu wa takwimu rasmi, Sudan ina wanajeshi zaidi ya 30,000 katika muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia. Gazeti la New York Times linaandika: Asilimia 40 ya wanajeshi na mamluki wanaopigana vita huko Yemen chini ya muungano vamizi wa kijeshi ni vijana na mabarobaro waliopatiwa mafunzo katika maeneo ya mpakani ya Saudia na kisha kugawanywa katika vikosi vya kijeshi.

Katika miezi ya hivi karibuni kuendelea kuweko majeshi ya Sudan katika muungano vamizi wa Saudi Arabia na kushirikiana na Riyadh katika vita vya Yemen, mgogoro wa Libya na kadhalika kukubali viongozi wa Khartoum kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel ni mambo ambayo Marekani na washirika wake wamekuwa wakiyatumia kuwashinikiza maradufu viongozi wa serikali ya mpito ya Khartoum ili wakubaliane nayo.

Amjad Farid, Naibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok anasema kuhusiana na jambo hilo kwamba, hakuna sababu yoyote ya kuifanya Sudan iwe katika nafasi ya vita na nchi yoyote ile.

Abdalla Hamdok, Waziri Mkuu wa Sudan

 

Licha ya kuwa viongozi wa Sudan bado hawajakubali kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel, lakini wamekuwa wakifanya juhudi ili kunufaika kadiri inavyowezekana na suala la kuendelea kuweko majeshi ya nchi hiyo huko Yemen. Filihahi majeshi ya Sudan hayashiriki katika vita vya Yemen tu bali yapo pia katika mgogoro wa Libya na inaonekana kuwa, askari hao ni wenzo na chombo cha kufanyia muamala pande mbili.

Kwa upande mmoja Saudia na waitifaki wake wanafanya hima ya kubakishwa vikosi hivyo ili kulinda nafasi yao ya sasa na hivyo wasiendelee kushindwa zaidi. Ama katika upande wa pili, serikali ya muda ya Sudan imeweka sharti la kubakia majeshi yake huko kwamba, ni kupatiwa misaada ya kifedha na himaya na uungaji mkono wa kisiasa.

Hivi sasa sambamba na kuweko ishara zote za kushindwa na kudhoofika majeshi ya Saudia katika vita vya Yemen, Khartoum nayo imeamua kutangaza habari ya kupunguza idadi ya askari wake katika nchi hiyo. Hata hivyo inaonekana kuwa, hatima ya uamuzi wa jambo hilo bado ni tata na isiyoeleweka..

Tags