Uchumi wa Afrika kupungua kwa asilimia -3.3 mwaka 2020
Ustawi wa uchumi katika eneo la Afrika kusini mwa jangwa la Sahara unakadiriwa kuwa hasi kwa asilimia -3.3 kwa mwaka huu kutokana na athari za virusi vya Corona.
Hayo yamo kwenye ripoti mpya ya Benki ya Dunia ambayo imeongeza kuwa hii itakuwa ni mara ya kwanza uchumi wa Afrika kudorora baada ya miaka 25 huku ikitabiriwa kuwa janga la Corona litapelekea watu milioni 40 kutumbukia katika umasikini barani Afrika mwaka 2020.
Ripoti hiyo imesema, janga la Corona limekuwa na athari kubwa katika shughuli za kiuchumi katika eneo la Afrika kusini mwa jangwa la Sahara, na kuhatarisha maendeleo makubwa ya kiuchumi yaliyopatikana kwenye eneo hilo katika mwongo mmoja uliopita.
Kutokana na ripoti hiyo, pato halisi la ndani la Afrika kusini mwa Sahara linakadiriwa kufikia asilimia 2.1 mwaka ujao, ambalo ni chini ya kiwango kilichofikiwa mwaka 2019, kwa matarajio kuwa kesi mpya za virusi vya Corona zitaendelea kupungua katika eneo hilo na maambukizi mapya hayatasababisha kufungwa kwa shughuli za kibiashara na kijamii.

Ripoti hiyo imesema nchi kama vile Angola na Nigeria zitaathirika vibaya kiuchumi kutokana na kutegemea sana mauzo ya mafuta katika soko la kimataifa ambapo bei ya bidhaa hiyo imepungua sana.
Hata hivyo nchi kama vile Ivory Coast, Ethiopia na Kenya ambazo hazitegemei sana mauzo ya mali ghafi nje ya nchi zinatazamiwa kuendelea kushuhudia ustawi wa kiuchumi ingawa utakuwa wa kiwango cha chini. Nazo nchi kama vile Cabo Verde, Mauritius na Usheliheli ambazo hutegemea sana utalii pia zitakumbwa na matatizo makubwa kufuatia kupungua kwa kiwango kikubwa watalii.