Magaidi kadhaa wa al-Shabaab wauawa kusini mwa Somalia
Wanachama watano wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab wameangamizwa katika operesheni ya jeshi la Somalia katika mji wa Dinsor, eneo la Bay kusini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Shine Mayow, Kamanda wa Kikosi cha Jimbo la Kusini Magharibi katika mji wa Dinsor amesema mbali na wanamgambo watano wa al-Shabaab kuuawa, wengine kadhaa wamejeruhiwa katika operesheni hiyo.
Amebanisha kuwa, wamefanikiwa kuwafarusha katika mji huo wanachama wengine wa genge hilo la kigaidi lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda.
Mapema mwezi huu, magaidi wasiopungua wanane waliuliwa katika operesheni ya mashambulio iliyofanywa na jeshi la Somalia kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu.
Vikosi vya serikali ya Somalia hivi karibuni vimeimarisha operesheni dhidi ya genge la al-Shabaab kwenye maeneo ya katikati na kusini mwa nchi hiyo.
Tangu mwaka 2007 kundi la kigaidi la al-Shaabab limekuwa likifanya operesheni za hujuma na mashambulio kwa lengo la kuiangusha serikali ya Somalia.