Maandamano ya kutaka kuvunjwa kikosi katili cha polisi Nigeria yashtadi
Maandamano ya nchi nzima ya wananchi wa Nigeria wanaotaka kuvunjwa Kikosi Maalumu cha Kupambana na Ujambazi (SARS) cha Jeshi la Polisi yamechachamaa.
Mtu mmoja ameripotiwa kuuawa katika maandamano hayo katika mji wa Ogbomoso, jimboni Oyo. Askari polisi wametumia risasi hai na mabomu ya kutoa machozi kwa lengo la kuzima maandamano hayo katika baadhi ya majimbo ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Baadhi ya waandamanaji hao walikuwa wamebeba mabango yenye jumbe zisemazo: Tumechoka, Maliza SARS, Polisi Wanawaibia Vijana, Mimi si Mhalifu na Maisha Yetu ni Muhimu.
Maandamano hayo yameshika kasi zaidi katika mji wa Lagos na maeneo yanayouzunguka kama vile Ikoyi, Amuwo-Odofin, Ikorodu, Unilag, Ajegunle, Egbeda, Agege, Gbagada, Bariga, Ikotun, Idimu, Lekki, na Yaba.
Waandamanaji hao wamesema Kikosi Maalumu cha Kupambana na Ujambazi (SARS) cha Jeshi la Polisi kinawalenga vijana na kutishia kuwaua iwapo hawatakubaliana na agizo lao la kuwapa pesa.
Maandamanao haya ya kulaani ukatili wa polisi ya Nigeria yameratibiwa kufanyika pia katika nchi mbalimbali duniani kama vile Marekani, Uingereza, Ujerumani, Uswisi na Canada.