Watu 10 wauawa Nigeria katika maandamano ya kulaani ukatili wa polisi
Watu wasiopungua 10 wameuawa Nigeria katika maandamano ya kulaani ukatili na ukandamizi unaotekelezwa na polisi ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, Polisi ya Nigeria imetumia nguvu ziada dhidi ya waandamanaji wasio na silaha tokea maandamano hayo yaanze Alhamisi.
Katika taarifa siku ya Jumanne, Shirika hilo limesema Polisi ya Nigeria imeua waandamanaji wasiopungua 10 tokea yaanza maandamano ya kupinga ukatili wa Kikosi Maalumu cha Kukabiliana na Wizi (SARS).
Kikosi hicho cha Polisi ya Nigeria kinahusishwa na ukatili mkubwa na kupelekea Wanigeria waingiwe na hasira na kujitokeza mitaani kote katika nchi hiyo wakitaka kivunjwe. Idara ya Polisi Nigeria imesema kikosi hicho sasa kitavunjwa.
Amnesty International imesema kuwa kitendo cha Polisi ya Nigeria cha kukandamiza maandamano kwa kutumia nguvu ziada ni ishara ya namna maafisa wa usalama wa Nigeria wanavyopuuza haki ya uhai. Shirika hilo la kutetea haki za binaamu limeonya kuwa utumizi wa nguvu ziada dhidi ya raia ni jinai kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Polisi ya Nigeria imesema maafsia wa kikosi kilichovunjwa cha SARS watachunguzwa kiakili kabla ya kuingizwa katika kikosi kipya kitakachojulikana kama SWAT.
Ikumbukwe kuwa Agosti 22 maafisa wa usalama wa Nigeria waliwashambulia wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria waliokuwa wakishiriki katika mambolezo ya mwezi wa Muharram mwaka huu wa 1422 Hijria ambapo waumini watatu waliuawa. Tokea mwaka 2015, maafisa wa usalama wa Nigeria wameua mamia ya wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria huku kiongozi wa harakati hiyo Sheikh Ibrahim Zakkzaky akiendelea kushikiliwa korokoroni kinyume cha sheria.