Watu kadhaa wauawa na kujeruhiwa katika maandamano ya ghasia Sudan
Watu kadhaa wameuawa na kujeruhiwa katika maandamano ya ghasia huko mashariki mwa Sudan.
Shirika la habari la Anadolu limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, watu saba wameuawa na wengine 270 wamejeruhiwa katika makabiliano baina ya waandamanaji na maafisa usalama katika mkoa wa Kassala, mashariki mwa Sudan usiku wa kuamkia leo.
Kufuatia machafuko hayo, serikali ya Sudan imetangaza marufuku ya kutoka nje nyakati za usiku katika mkoa huo, huku kamati ikiundwa kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo.
Juzi Jumatano pia, watu sita waliuawa huku wengine 20 wakijeruhiwa katika ghasia zilizoshuhudiwa katika mji wa Sawakin ulioko katika mkoa huo huo wa Kassala.
Sudan katika miezi ya hivi karibuni imekabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi, huku bei za bidhaa kama mkate, unga, fueli na gesi zikipanda kutokana na kuongezeka thamani ya dola ya Marekani mkabala wa sarafu ya nchi hiyo.
Serikali ya mpito ya Sudan inayoongozwa na Waziri Mkuu, Abdallah Hamdok inatazamiwa kusalia madarakani kwa kipindi cha miezi 39 kuanzia Agosti 21 mwaka jana, hadi uchaguzi mkuu utakapofanyika mwishoni mwa mwaka 2022.