Bensouda kwenda Sudan, ataka al Bashir akabidhiwe kwa mahakama ya ICC
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) anatarajiwa kuelekea nchini Sudan kwa ajili ya kuchunguza suala la kukabidhiwa rais wa zamani wa nchi hiyo, Omar al Bashir kwa mahakama hiyo iliyoko The Hague nchini Uholanzi.
Fatou Bensouda anatarajiwa kukutana na maafisa wa serikali ya Sudan na kubadilishana mawazo juu ya suala la kukabidhiwa rais wa zamani wa nchi hiyo, Omar Hassan al Bashir kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu.
Duru za habari zinasema, katika safari hiyo Bensouda atajaribu kuwashawishi viongozi wa Sudan waafiki suala la kukabidhiwa al Bashir na maafisa wengine kadhaa wa zamani wa nchi hiyo ili wahukumiwe katika mahakama ya kimataifa ya ICC.
Awali baraza la kijeshi la serikali ya mpito ya Sudan lilikuwa limetangaza kuwa, nchi hiyo haitamkabidhi Omar al Bashir kwa taasisi yoyote ya kigeni na kwamba kiongozi huyo wa zamani wa Sudan atahukumiwa ndani ya nchi.
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) inamtuhumu Omar al Bashir kwamba alihusika na mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa eneo la Darfur huko magharibi mwa Sudan na vilevile kutenda jinai dhidi ya binadamu na imetoa kibali cha kutiwa nguvuni mtuhumiwa huyo.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema watu laki tatu waliuawa na wengine wasiopungua milioni mbili walilazimika kuwa wakimbizi katika vita vya serikali ya Sudan dhidi ya waasi wa Darfur vilivyoanza mwaka 2003.