AU yatakiwa iingilie kati mgogoro wa Nigeria, ECOWAS yatoa neno
Asasi za kiraia na mashirika ya kutetea haki za binadamu yametoa mwito kwa Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini kama Mwenyekiti wa mzunguko wa Umoja wa Afrika, kuingilia kati mgogoro na machafuko ya umwagaji damu yanayoendelea kushuhudiwa nchini Nigeria.
Ramaphosa ametakiwa kuliwasilisha suala hilo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuitisha mkutano wa dharura na Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika Magharibi (ECOWAS), ili kuhakikisha kuwa uthabiti wa eneo hilo hauyumbishwi na machafuko hayo ya Nigeria.
Wakati huohuo, Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika Magharibi (ECOWAS) imevitaka vyombo vya usalama vya Nigeria vijizuie kutumia nguvu kupita kiasi katika kuzima maandamano hayo ya wananchi.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema watu zaidi ya 20 wameuawa katika maandamano hayo yanayoshuhudiwa kwa siku kadhaa sasa katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Kwa zaidi ya wiki mbili sasa, maelfu ya raia wa Nigeria wamekuwa wakiandamana kote nchini humo dhidi ya ukatili unaofanywa na Kikosi Maalum cha Kupambana na Ujambazi (SARS), hata baada ya serikali kudai kuwa imekivunja.
Sheria ya kutotoka nje imetangazwa katika mji wa Lagos nchini Nigeria huku ghasia zikienea nchini humo kupinga ukatili wa polisi hususan dhidi ya tabaka la vijana.