Ujumbe wa Wazayuni wakaribishwa Sudan kwa maandamano ya upinzani
(last modified Thu, 22 Oct 2020 07:56:25 GMT )
Oct 22, 2020 07:56 UTC
  • Ujumbe wa Wazayuni wakaribishwa Sudan kwa maandamano ya upinzani

Ujumbe wa ngazi za juu wa utawala wa Kizayuni wa Israel umekaribishwa kwa maandamano ya upinzani nchini Sudan.

Mtu mmoja ameuawa huku wengine 14 wakijeruhiwa katika maandamano hayo ya jana mjini Khartoum, ya kupinga njama za chini kwa chini za kuanzisha uhusiano wa kawaida kati ya Sudan na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Shirika la habari la Anadolu la Uturuki limenukuu mtandao wa habari wa Kizayuni wa Walla ulioripoti kuwa, ndege ya kibinafsi inayotumiwa na maafisa wa Israel ilitua jana katika uwanja wa ndege mjini Khartoum, na kisha ikaondoka masaa machache baadaye.

Habari zaidi zinasema kuwa, wakati ndege hiyo ikitua Khartoum, Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alikuwa akitoa hotuba juu ya Sudan.

Pomeo na Abdallah Hamdok, Waziri Mkuu wa Sudan

Khartoum inaandamwa na mashinikizo ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Tel Aviv, baada ya kuondolewa jina la Sudan katika orodha ya Marekani ya nchi eti zinazounga mkono ugaidi. 

Wananchi na makundi ya Sudan yanapinga vikali kuanzishwa uhusiano kati ya nchi hiyo na utawala wa Kizayuni, kufuata mkumbo wa Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain.

Tags