Ethiopia yamwita kumsaili balozi wa Marekani kwa matamshi aliyotoa Trump
(last modified Sat, 24 Oct 2020 14:41:15 GMT )
Oct 24, 2020 14:41 UTC
  • Ethiopia yamwita kumsaili balozi wa Marekani kwa matamshi aliyotoa Trump

Balozi wa Marekani mjini Addis Ababa ameitwa kusailiwa kufuatia kauli aliyotoa Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu bwawa la An-Nahdhah au Renaissance.

Serikali ya Ethiopia imemwita kumsaili balozi wa Marekani nchini humo Michael Raynor na kumtaka atoe maelezo kufuatia maneno aliyosema Trump kuhusiana na kuripuliwa bwawa la An-Nahdhah.

Katika matamshi yake ya kwanza aliyotoa kuhusu kadhia ya bwawa la An-Nahdhah lililojengwa na Ethiopia na ambalo limezusha mvutano, Rais Donald Trump wa Marekani alisema jana kuwa, kuna uwezekano Misri ikaliripua bwawa hilo.

Nchi tatu za Afrika za Misri, Ethiopia na Sudan zinatafautiana kuhusu haki ya kila moja katika maji ya Mto Nile pamoja na mgao wa kila nchi kwa maji ya mto huo.

Bwawa la Renaissance

Ethiopia ilianza ujenzi wa bwawa la An-Nahdhah kwenye maji ya Mto Nile Aprili 2011.

Kulingana na ratiba ya awali, shughuli ya ujazaji maji ya mto huo katika bwawa la Renaissance ilikuwa ianze mwaka 2017 lakini iliakhirishwa hadi mwaka huu kutokana na hitilafu kali zilizozuka baina ya Ethiopia, Misri na Sudan.

Hivi karibuni mivutano hiyo ya maneno kuhusiana na bwawa hilo iligeuka kuwa ya vitisho vya makabiliano ya kijeshi kati ya nchi hizo hususan baina ya Misri na Ethiopia.../

Tags