Mpinzani wa Rais Museven, Bobi Wine akamatwa baada ya kupasishwa kugombea urais
-
Bobi Wine
Kiongozi wa Jukwaa la Umoja wa Kitaifa anayebeba bendera ya chama hicho katika uchaguzi ujao wa rais nchini Uganda, Robert Kyagulanyi maarufu kwa jina la Bobi Wine amekamatwa muda mfupi baada ya kupasishwa kugombea kiti hicho.
Ripoti zinasema kuwa, dirisha la gari la Bobi Wine lilivunjwa kabla ya kutolewa nje na kuwekwa kwenye gari nyeusi iliyokuwa ikingojea eneo hilo.
Mapema leo Tume ya Uchaguzi ya Uganda ilikuwa imempasisha Bobi Wine kugombea katika uchaguzi wa rais wa 2021 baada ya kukamilisha taratibu zinazohitajika.
Katika hotuba yake ya kwanza baada ya kupasishwa kugombea urais mwaka ujao, Bobi Wine amemuonya Rais Yoweri Museveni na Tume ya Uchaguzi kuhusu kile alichosema ni "kucheza na matokeo ya uchaguzi".
Hadi sasa wagombea 10 wamepasishwa kuwania kiti cha rais nchini Uganda akiwemo kamanda wa zamani wa Jeshi, Mugisha Muntu na aliyekuwa Waziri wa Usalama Jenerali Henry Tumukunde.
Wagombea hawa watachuana na Rais Yoweri Kaguta Museveni mwenye umri wa miaka 76 ambaye anaiongoza Uganda kwa zaidi ya miaka 30.
Mwaka 2017 Bunge la Uganda lilipiga kura ya kuondoa ukomo wa umri wa miaka 75, na kumtengenezea Museveni ambaye sasa ana umri wa miaka 76, njia ya kuwania urais katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mapema mwakani.