Uganda yatangaza tarehe ya uchaguzi mkuu, kampeni kuanza Jumatatu
Tume ya Uchaguzi Uganda (EC) imetangaza tarehe 14 Januari mwaka ujao 2021 kuwa siku ya kufanyika uchaguzi mkuu ukiwemo wa urais.
Mwenyekiti wa tume hiyo, Hakimu Simon Byabakama amesema kampeni za uchaguzi huo mkuu wa Uganda zitaanza kutifua vumbi Jumatatu ijayo ya Novemba 9, na zitaendelea hadi Januari 12 mwakani.
Hakimu Byabakama amesema wagombea wako huru kuzindua manifesto na ilani za vyama vyao kabla ya kuanza kampeni Jumatatu ijayo.
Hadi sasa wagombea 10 wamepasishwa kuwania kiti cha rais nchini Uganda akiwemo mbunge Robert Kyagulanyi maarufu kwa jina la Bobi Wine wa chama cha NUP, kamanda wa zamani wa Jeshi, Mugisha Muntu na aliyekuwa Waziri wa Usalama Jenerali Henry Tumukunde.
Wagombea hawa watachuana na Rais Yoweri Kaguta Museveni mwenye umri wa miaka 76 ambaye anaiongoza Uganda kwa zaidi ya miaka 30.
Mwaka 2017 Bunge la Uganda lilipiga kura ya kuondoa ukomo wa umri wa miaka 75, na kumtengenezea Museveni ambaye sasa ana umri wa miaka 76, njia ya kuwania urais katika uchaguzi huo wa mapema mwakani.
Katika hatua nyingine, chama cha upinzani cha NUP ambacho kilikuwa kinatazamiwa kuzindua ilani yake kesho Ijumaa, kimeakhirisha shughuli hiyo hadi Jumamosi, kufuatia kifo cha ghafla cha mwanachuoni maarufu wa Kiislamu nchini humo, Sheik Annas Kaliisa, ambaye atazikwa hiyo kesho.