Sudan yatoa msamaha kwa watu wote waliobeba silaha kinyume cha sheria
Mkuu wa Baraza la Utawala la Sudan ametangaza msamaha kwa watu wote waliokuwa wamebeba silaha kinyume cha sheria.
Kwa mujibu wa amri iliyotolewa na Luteni Jenerali Abdel Fattah al Burhan, msamaha huo unajumuisha watu wote waliobeba silaha na kushiriki katika operesheni yoyote ya kijeshi, kuingia vitani au kushiriki kwenye operesheni yoyote inayohusiana na vita.
Al Burhan amesisitiza kuwa, msamaha huo hata hivyo, hauhusishi watu ambao wameshatolewa waranti wa kukamatwa ili wakabidhiwe kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.
Aidha hautawahusisha watu ambao wanakabiliwa na tuhuma au mashtaka yanayohusu jinai za mauaji ya kimbari au jinai dhidi ya binadamu au waliokwisha tolewa hukumu maalumu na kisasi dhidi yao.
Sudan imeshuhudia machafuko na mivutano mikali tangu alipoondolewa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo Omar al Bashir na hatamu za nchi kushikiliwa na serikali ya mpito.
Al Bashir aling'olewa uongozini Aprili mwaka 2019 baada ya maandamano makubwa ya upinzani wa wananchi na uingiliaji kati wa jeshi; na hivi sasa Sudan inaongozwa na serikali ya mpito iliyo chini ya Baraza la Utawala linaloongozwa na Luteni Jenerali Abdel Fattah al Burhan.../