Sudan yakadhibisha safari ya ujumbe wa Israel mjini Khartoum
(last modified Sun, 15 Nov 2020 11:48:54 GMT )
Nov 15, 2020 11:48 UTC
  • Sudan yakadhibisha safari ya ujumbe wa Israel mjini Khartoum

Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imekadhibisha taarifa kuwa ilifahamu juu ya safari ya ujumbe wa utawala haramu wa Israel katika mji mkuu wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, Khartoum.

Gazeti la Sharq al-Awsat limemnukuu Omar Qamaruddin, Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan akisema hayo na kuongeza kuwa, Baraza la Uongozi la nchi hiyo halikuwa na ufahamu juu ya safari ya leo ya ujumbe wa utawala haramu wa Israel mjini Khartoum.

Wiki iliyopita, gazeti hilo lilinukuu duru zilizo karibu na serikali ya Sudan zikisema kuwa, ujumbe utakaoenda Khartoum leo Jumapili unajumuisha watu wenye uraia mbalimbali wakiwemo Wazayuni.

Hii ni katika hali ambayo, muungano wa vyama vya siasa vya Sudan vinavyopinga nchi hiyo kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel umesema, upinzani wa wananchi kwa suala hilo ni mkubwa mno kwa kiwango ambacho haikutarajiwa.

Wasudan katika maandamano ya kuonyesha uungaji mkono kwa Palestina

Tarehe 23 ya mwezi uliopita wa Oktoba, Wizara ya Mambo ya nje ya Sudan ilitangaza kuwa serikali ya mpito ya nchi hiyo imeafiki kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel na hivyo kuifanya Sudan nchi ya tano baada ya Misri (1979), Jordan (1994), Imarati na Bahrain (2020) kufikia mapatano na Israel na kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo wa Kizayuni.

Kufuatia kutangazwa uamuzi wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel, makundi mbalimbali ya kisiasa nchini Sudan yamepinga vikali makubaliano hayo, vikiwemo vyama washirika katika muungano unaotawala nchi hiyo.

Tags