Sudan yasusia kikao cha kujadili bwawa la al Nahdha
Sudan imesusia kushiriki katika kikao cha mawaziri cha kujadili mradi wa bwawa la al Nahdha la nchini Ethiopia, ikiwa ni kulalamikia jinsi mazungumzo yanavyoendeshwa na nchi tatu za Ethiopia, Misri na Sudan.
Jana Jumamosi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan ilitoa taarifa na kusema kwamba, Khartoum iimeamua kususia kikao cha nchi tatu za Ethiopia, Misri na Sudan kuhusu bwawa la al Nahdha kwani hairidhishwi na jinsi mazungumzo hayo yanavyoendeshwa.
Yasir Abbas, Waziri wa Maji wa Sudan amemwandikia barua waziri mwenzake wa Ethiopia, Seleshi Bekele akitaka wataalamu wa Umoja wa Afrika wapewe nafasi zaidi ya kusahilisha uendeshaji wa mazungumzo baina ya nchi hizo tatu, kupunguza nyufa na mivutano na kuondoa manung'uniko. Katika barua yake hiyo kwa waziri mwenzake wa Ethiopia, Waziri wa Maji wa Sudan amesema, kutopewa nafasi kubwa zaidi wataalamu wa AU ndiko kulikopelekea kuvunjika na kutokuwa na natija mazungumzo yote yaliyofanyika hadi hivi sasa kuhusu bwawa la al Nahdha.
Katika barua yake hiyo, kwa mara nyingine Sudan imetilia mkazo wajibu wa kusimamiwa na Umoja wa Afrika; mazungumzo yanayohusiana na bwawa la al Nahdha, lililozua mgogoro mkubwa baina ya nchi tatu za Ethiopia, Misri na Sudan.
Bwawa la al Nahdha limejengwa katika umbali wa kilomita 15 kutoka kwenye mpaka wa Ethiopia na Sudan. Hadi mwezi Oktoba 2019, ujenzi wa bwawa hilo ulikuwa umeshamalizika kwa asilimia 70. Litakapoanza kufanya kazi bwawa hilo, litakuwa kituo kikuu zaidi cha kuzalisha umeme kwa kutumia maji, duniani.
Serikali ya Cairo inalalamika kuwa, bwawa hilo litapunguza kiwango cha maji ya Mto Nile yanayoelekea Misri. Hata hivyo Ethiopia inasema, kila nchi ina haki ya kutumia rasilimali zake kuwaletea ustawi na maendeleo watu wake.