Sudan yakiri rasmi kutembelea nchi hiyo ujumbe wa utawala wa Kizayuni
Msemaji wa Baraza la Uongozi la Sudan jana Jumapili alithibitisha habari ya kutembelewa nchi hiyo na ujumbe wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Hayo yameripotiwa na gazeti la Rai al Yaum ambalo limemnukuu Muhammad al Faki akithibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, ujumbe huo wa Israel ulionana na viongozi wa ngazi za juu wa Sudan mjini Khartoum.
Amedai kuwa, lengo la ziara ya ujumbe huo wa Israel mjini Khartoum lilikuwa la kijeshi tu na ndio maana ulionana na maafisa wa ngazi za juu wa kijeshi.
Msemaji huyo wa Baraza la Uongozi la Sudan pia amesema, ujumbe huo wa Israel ulianza kwa kutembelea mfumo wa kujilinda na mashambulizi ya anga wa vikosi vya ulinzi vya Sudan na ingawa ujumbe huo ulionana na maafisa wa ngazi za juu wa Sudan, lakini hawakujadiliana uhusiano wa kisiasa wa pande mbili.
Awali viongozi wa Sudan walikanusha kutembelewa nchi hiyo na ujumbe wowote ule wa utawala dhalimu wa Israel. Lakini sasa wamekiri wakidai kuwa haukuhusiana na masuala ya kisiasa.
Tarehe 23 Oktoba 2020, Baraza la Uongozi la Sudan linaloongozwa na Luteni Jenerali Abdel Fattah al Burhan lilitangaza uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel, licha ya upinzani mkubwa wa wananchi, vyama na asasi mbalimbali za Sudan.
Hadi leo hii upinzani wa wananchi wa Sudan kwa hatua hiyo ya kujidhalilisha kwa Wazayuni unaendelea na mara kwa mara viongozi wa serikali ya mpito ya Sudan wanafanya juhudi za kutetea na kuhalalisha hatua yao hiyo.