Marekani kuondoa wanajeshi wake Somalia kufikia Januari 2021
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i65017-marekani_kuondoa_wanajeshi_wake_somalia_kufikia_januari_2021
Maafisa wa kijeshi wa Marekani wametangaza kuwa, majeshi ya nchi hiyo yaliyoko nchini Somalia muda si mrefu yataondoka katika nchi hiyo ya pembe ya Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 05, 2020 04:13 UTC
  • Marekani kuondoa wanajeshi wake Somalia kufikia Januari 2021

Maafisa wa kijeshi wa Marekani wametangaza kuwa, majeshi ya nchi hiyo yaliyoko nchini Somalia muda si mrefu yataondoka katika nchi hiyo ya pembe ya Afrika.

Maafisa hao wa kijeshi wanasema kuwa, asilimia kubwa ya askari wa Marekani walioko Somalia watakuwa wameondoka nchini humo ifikapo tarehe 15 Januari ya mwaka ujao wa 2021.

Tayari Rais Donald Trump ameitaka Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo Pentagon sambamba na kuondoa nchini Somalia sehemu kubwa ya askari hao na kuwarejesha nyumbani, iunde kikosi kidogo kitakachobakia katika mji mkuu Mogadishu.

Ripoti zinaonyesha kuwa, kwa sasa Marekani ina askari 700 nchini Somalia. Viongozi wa mataifa ya Afrika ikiwemo Somalia daima wamekuwa wakitaka majeshi ya Marekani yaondoke katika nchi zao.

Wanamgambo wa al-Shabab wa Somalia wenye mfungano na mtandao wa al-Qaeda

 

Viongozi wa mataifa ya Afrika wanaamini kuwa, kuendelea kuwepo askari wa Marekani katika nchi zao hakuna kitu kingine ghairi kuzidi kuvuruga amani na usalama sambamba na kuenea harakati za makundi ya kigaidi.

Askari wa Marekani wapo nchini Somalia kwa kisingizio cha kuvisaidia vikosi vya serikali ya Mogadishu katika operesheni zake za kukabiliana na wanamgambo wa kundi la al-Shabab.

Tangu mwaka 2007, kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa al-Qaida limekuwa likifanya mashambulizi ndani ya Somalia kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya nchi hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.