Katibu Mkuu wa UN alaani hujuma dhidi ya shule Nigeria
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali hujuma iliyofanywa Ijumaa iliyopita katika shule ya sekondari mkoani Katsina nchini Nigeria, ambapo mamia ya wavulana walitekwa nyara na wahalifu waliokuwa na silaha.
Msemaji wa Katibu Mkuu huyo Stephane Dujarric amesema, Guterres ametaka watoto hao waliotekwa nyara waachiliwe mara moja, na kurudishwa salama kwa familia zao.
Pia katibu mkuu huyo amesisitiza kuwa, mashambulizi dhidi ya shule na taasisi nyingine za elimu ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, na akazitaka mamlaka nchini Nigeria kuwafikisha wahusika wa shambulizi hilo mbele ya sheria.
Wakati huo huo, Gavana wa Jimbo la Katsina la Nigeria Aminu Masari amesema, wapatanishi wa mazungumzo wa serikali wanawasiliana na wateka nyara wa wanafunzi 333 wa shule ya sekondari huko Katsina, kaskazini magharibi mwa Nigeria. Lakini amekataa kudokeza habari zaidi halisi kuhusu mazungumzo hayo wakati viongozi wanajaribu kuwalinda wahanga na kuwaokoa.

Hii si mara ya kwanza majambazi kuwateka wanafunzi nyara kutoka shuleni. Mbinu hiyo ilishawahi kutumiwa na makundi ya zamani kama vile magaidi wakufurishaji wa Boko Haram, hali ambayo imezusha hofu kwamba makundi ya wahalifu kaskazini -magharibi mwa Nigeria sasa yanaiga magaidi hao wakufurishaji.