Watu karibu 80 wauawa katika mashambulio ya wabeba silaha Niger
(last modified Sun, 03 Jan 2021 03:20:00 GMT )
Jan 03, 2021 03:20 UTC
  • Watu karibu 80 wauawa katika mashambulio ya wabeba silaha Niger

Makumi ya watu wameuawa katika mashambulio mawili yanayosadikika kutekelezwa na makundi ya kigaidi huko nchini Niger.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, magenge hayo ya kigaidi yameshambulia vijiji viwili na kuua watu 79 na kujeruhi wengine wengi, katika mpaka wa Niger na Mali.

Duru za habari zinaarifu kuwa, magaidi hao walishambulia kijiji cha Tchombangou na kuua watu 49 mbali na kujeruhi wengine 17, huku watu wengine 30 wakiuawa katika shambulio la pili dhidi ya kijiji cha Zaroumdareye, katika mpaka wa magharibi wa Niger na Mali.

Alkache Alhada, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Niger amethibitisha habari za kutokea mashambulio hayo, ingawaje hajasema idadi ya waliouawa au kujeruhiwa katika hujuma hizo. Hata hivyo amesisitiza kuwa, wanajeshi wa nchi hiyo wametumwa kwenda kuimarisha doria katika maeneo yaliyoshambuliwa.

Mapema jana, Ufaransa ilisema kuwa wanajeshi wake wawili wameuawa katika hujuma ya kigaidi nchini Mali, masaa machache baada ya kundi moja lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda kudai kuwa lilihusika na shambulio jingine lililouawa askari watatu wa nchi hiyo ya Ulaya Jumatatu iliyopita.

Niger inasumbuliwa na hujuma za kigaidi licha ya uwepo wa askari ajinabi

Katikati ya mwezi uliopita wa Disemba, shambulio lililofanywa na magaidi wa Boko Haram liliuawa watu wasiopungua 27 na kujeruhi wengine kadhaa katika kijiji cha Toumour katika eneo la Diffa huko nchini Niger. 

Katika miezi ya hivi karibuni maeneo ya magharibi mwa Niger yamekuwa yakisumbuliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya makundi ya kigaidi. 

 

Tags