Wananchi wa Uganda wapiga kura, wasubiri matokeo, wapinzani walalamika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i65768-wananchi_wa_uganda_wapiga_kura_wasubiri_matokeo_wapinzani_walalamika
Mamilioni ya watu wa Uganda leo wamejitokeza na kushiriki kwenye zoezi la kupiga kura baada ya kampeni zilizogubikwa na ghasia.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Jan 14, 2021 10:06 UTC
  • Wananchi wa Uganda wapiga kura, wasubiri matokeo, wapinzani walalamika

Mamilioni ya watu wa Uganda leo wamejitokeza na kushiriki kwenye zoezi la kupiga kura baada ya kampeni zilizogubikwa na ghasia.

Katika uchaguzi wa leo kumeshuhudiwa mchuano mkali baina ya Rais Yoweri Museveni mwenye umri wa miaka 76, ambaye amekuwa madakrani kwa miaka 35, na msanii Robert Kyagulanyi Ssentamu, ambaye ni maarufu kama Bobi Wine mwenye umri wa miaka 38.

Wapigakura zaidi ya milioni 17 walitarajiwa kupiga kura kuamua ni yupi kati ya wagombea hao atachukua hatamu za uongozi.

Kampeni za uchaguzi ambazo zilimalizika siku ya Jumatano wiki hii zilikumbwa na vurugu ambazo zilisababisha vifo vya watu kadhaa, wengi kutoka kambi ya upinzani.

Wakati huo huo mamia ya wanajeshi wameshika doria katika barabara za mji mkuu Kampala na miji kadhaa "kudumisha utulivu", mamlaka zimesema. Serikali inataka kuepuka vurugu zaidi, kama ile iliyoikumba nchi hiyo mnamo mwezi Novemba 2020.

Serikali ya Rais Museveni ilifunga mtandao wa intaneti jioni ya jana, saa chache kabla upigaji kura kuanza katika kile ambacho kimetajwa kuwa ni hatua ya kudumisha usalama.

Wananchi wa Uganda wakisubiri kupiga kura

Wagombea 11 wanawania kiti cha urais wakiwemo wanajeshi wawili wastaafu ambao wamemgeukia mkuu wao wa zamani, Museveni. Lakini ni Wine pekee ambaye jina lake hasa ni Robert Kyagulanyi ndiye anayesemekana kuwa na nafasi nzuri zaidi ya kumshinda Museveni. Leo pia mbali na kumchagua rais watu wa Uganda wamepiga kura kuwachagua wabunge wa bunge la kitaifa.

Wakati huo huo, Mugisha Muntu, mgombea urais kwa tiketi ya chama cha National Transformation, amelalamika kuwa maajenti wake wamekamatwa huko Jinja na Ntungamo.

Patrick Oboi Amuriat, mgombea wa chama cha Forum For Democratic Change, amedai uchaguzi wa leo umegubikwa  na wizi wa kura na hivyo hawatakubali matokeo.

Kwa upande wake  Bobi Wine, wa chama cha National Unity Platform amesema maajenti wa chama chake wamekamatwa maeneo mbali mbali ya Uganda.

Rais Yoweri Museveni amesema atakubali matokeo ya uchaguzi endapo atashindwa. Zoezi la upigaji kura lilimalizika saa 10 alasiri kwa saa za Uganda na matokeo yanatazamiwa kutangazwa baada ya masaa 48.