Waziri mwingine aaga dunia kwa corona nchini Zimbabwe
Zimbabwe imempoteza waziri wake wa pili ambaye ameaga dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Zimbabwe (ZBC), Ellen Gwaradzimbe, Waziri wa Masuala ya Mkoa wa Manicaland alifariki dunia mapema jana wakati walipokuwa akipokea matibabu katika hospitali moja ya nchi hiyo baada ya kuambukizwa virusi vya corona.
Mtoto wa kiume wa waziri huyo kwa jina la Rememberance amethibitisha habari hiyo ya kuaga dunia mamake aliyekuwa na umri wa miaka 60, kwa ugonjwa wa Covid-19.
Agosti mwaka uliopita wa 2020, Perrance Shiri, aliyekuwa Waziri wa Ardhi na Kilimo wa nchi hiyo aliaga dunia kwa maradhi hayo ya kuambukiza.
Mapema mwezi huu, serikali ya Zimbabwe ilitangaza kuwa sheria ya karantini ya nchi nzima imeanza kutekelezwa nchini humo kwa mara nyingine tena kutokana na kuongezeka maambukizi mapya ya corona. Sheria hiyo inatekelezwa baina ya Januari 5 hadi Januari 31.
Takwimu rasmi za karibuni zilizotangazwa na Wizara ya Afya ya Zimbabwe zinaonyesha kuwa, tangu kuenea maambukizi ya corona huko Zimbabwe had sasa watu 25,368 wameripotiwa kuambukizwa ugonjwa wa Covid-19 nchini humo; huku wengine 636 wakiaga dunia mwa ugonjwa huo.
Kadhalika watu zaidi ya 14,714 waliokuwa wameambukizwa maradhi hayo nchini humo wamepata afueni.