Wanajeshi wa Mali wauawa katika shambulio la wanamgambo wenye silaha huko Mopti
Wanajeshi kadhaa wa jeshi la Mali wameuawa na kujeruhiwa katika shambulio la wanamgambo wenye silaha katika jimbo la Mopti nchini humo.
Kanali Soulemane Dembele Msemaji wa Jeshi la Mali ameeleza kuwa, wanajeshi wao 9 wameuawa katika shambulio lililofanywa na karibu watu 20 katika eneo lililo karibu na kijiji cha Boni katika mkoa wa Mopti. Wanajeshi wengine 6 wa Mali wamejeruhiwa katika shambulio hilo la wanamgambo wenye silaha. Msemaji wa jeshi la Mali hata hivyo hakutaja utambulisho wa watu hao.

Mashambulizi ya makundi mbalimbali yenye misimamo mikali khususan wanachama wa mtandao wa kigaidi wa al Qaida na kundi la Daesh yameshtadi katika miezi ya karibuni katika maeneo mbalimbali huko Mali. Mashambulizi hayo yanajiri huko Mali katika hali ambayo wanajeshi wa Ufaransa wamepelekwa nchini humo kwa kisingizio ha kupambana na ugaidi.
Wananchi wa Mali wanalalamika kuwa, wanajeshi wa Ufaransa hawachukui hatua yoyote kufuatia kuongezeka hali ya machafuko na mashambulizi nchini humo.