Afrika Kusini yapiga marufuku chanjo ya corona kutoka Uingereza
Serikali ya Afrika Kusini imetangaza kusitisha mipango ya kuanza utoaji chanjo ya corona au COVID-19 kutoka Uingereza ya AstraZeneca na Oxford baada ya utafiti kubaini kuwa chanjo hiyo haiwezi kukabiliana na aina mpya ya corona iliyopatikana nchini humo.
Wiki iliyopita Afrika Kusini ilipokea dozi milioni moja ya chanjo ya AstraZeneca na Oxford na ikazindua zoezo la kuwachanja wahudumu wa afya. Hii ilikuwa chanjo ya kwanza ya COVID-19 kuanza kutumika nchini humo.
Kwa mujibu wa matokeo ya awali ya uchunguzi uliofanywa na wataalamu nchini humo, chanjo hiyo kutoka Uingereza haina manufaa kwa wagonjwa wa corona.
Matokeo ya utafiti huo mdogo uliofanywa na chuo kikuu cha Witwatersrand mjini Johannesburg, yamebaini kuwa chanjo ya AstraZeneca inatoa kinga ndogo tu dhidi ya "magonjwa mepesi na ya wastani" yanayosababishwa na aina mpya ya kirusi cha nchini Afrika Kusini.
Waziri wa afya wa Afrika Kusini Zweli Mkhize amesema chanjo ya AstraZeneca inaonekana kuwa na ufanisi dhidi aina ya awali ya kirusi cha corona lakini sio aina mpya ya kirusi cha corona kilichobadilika na kuibuka nchini humo. Kwa msingi huo, Afrika Kusini imetangaza kusitisha utoaji wa chanjo hiyo kwa muda.
Afrika Kusini inaongoza kwa maambukizi na vifo vya corona barani Afrika. Hadi sasa watu zaidi ya milioni 1.47 wameambukizwa corona nchini humo huku zaidi ya 46,000 wakiwa wamepoteza maisha.