Feb 09, 2021 06:27 UTC
  • Umoja wa Afrika waitaka Marekani ihitimishe vikwazo na mzingiro dhidi ya Cuba

Umoja wa Afrika umetaka kuhitimishwa vikwazo na mzingiro wa kiuchumi, kibiashara na kifedha iliowekewa Cuba kupitia amri ya utekelezaji iliyosainiwa mwaka 1962 na aliyekuwa rais wa wakati huo wa Marekani John F. Kennedy.

Katika kikao cha baraza la Umoja wa Afrika kilichohudhuriwa na viongozi wa nchi wanachama, Umoja wa Afrika umepitisha hati dhidi ya mzingiro huo ambao ulishadidishwa mwaka 2020 na aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump licha ya kuzuka janga la dunia nzima la mripuko wa virusi vya corona.

Viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika wamepitisha kwa mara ya 12 mfululizo azimio la kutaka kuondolewa mzingiro wa kiuchumi, kibiashara na kifedha, ambao Marekani imeiwekea Cuba, kikiwa ni kielelezo cha uungaji mkono wao kwa azimio lililoidhinishwa na Umoja wa Mataifa.

Mbali na kubainisha wasiwasi zilionao kutokana na kuendelezwa mzingiro huo, nchi wanachama wa AU zimeeleza kusikitishwa na kudorora tena uhusiano wa Washington na Havana katika kipindi cha miaka minne iliyopita na kuwatolea mwito viongozi wa Marekani wachukue hatua ya kuondoa vikwazo vilivyodumu kwa miaka mingi sasa.

Katika kipindi cha miaka minne ya utawala wake, aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump alirejesha tena vikwazo vya nchi hiyo dhidi ya Cuba.

Hii ni licha ya kwamba, katika mwaka wa mwisho wa utawala wa Barack Obama na baada ya kupita nusu karne, Marekani ilianzisha tena uhusiano wake wa kidiplomasia na Cuba na kuondoa baadhi ya vikwazo na vizuizi ilivyokuwa imeiwekea nchi hiyo.../   

Tags